Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, jana aliomba radhi Bunge baada ya kutoa kauli, iliyoonesha ubaguzi kwa wabunge kutoka Zanzibar.
Kabla ya kuomba radhi, kauli hiyo ilisababisha wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), kutoka nje ya Bunge kuonesha kukerwa na kauli hiyo.
Muda mfupi baadae, wabunge hao waliungwa mkono na wabunge kutoka Bara, ambao wanatoka Chadema na NCCR Mageuzi, ambao nao walitoka na kuwaacha wabunge wa CCM na mbunge wa UDP, John Cheyo.
Awali kabla ya kutoka nje, Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk (CUF), aliomba muongozo wa Spika akilalamikia kauli ya Werema wakati akimjibu Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF).
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar na sio katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa sio kila kitu kitaulizwa ndani ya bunge hilo.
Hoja ilianzia kwa Mnyaa, wakati akiomba Kamati ya Matumizi ya Bunge iliyokaa kupitisha vifungu vya hotuba Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2014/15.
Mbunge huyo aliituhumu Wizara ya Katiba na Sheria kuwa ni moja ya Wizara muhimu lakini imekuwa ikivunja sheria na haki za binadamu.
Baada ya hoja hiyo, Werema alijibu: “Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa sio mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu.”
Mara baada ya bunge kurejea, Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk (CUF), aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya ubaguzi.
“Mheshimiwa Spika, wakati wa majadiliano na wakati ambapo Mheshimiwa Mnyaa anaongea na kutaka ufafanuzi wa haki za binadamu, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Hata hivyo Spika alipinga na kusema; “hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini, umeendelea kuzungumza, tunaendelea Katibu.”
Baada ya kauli ya spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje wote kwa wakati mmoja na kuwaacha wabunge wenzao wa upinzani wakiendelea kuitana na kutafakari cha kufanya.
Spika alifafanua kuwa Mbarouk alikosea kumshutumua Spika hadharani, kwa kuwa kanuni zinaelekeza kama amekosea, malalamiko yapelekwe katika Kamati ya Kanuni.