“Ni kweli kwamba kutokuwapo kwao kunaweza kuwa na athari katika kufanya uamuzi, lakini pia hatuwezi kusema ni athari zipi kwa sasa kwa sababu hakuna suala ambalo linapaswa kufanyiwa uamuzi kwa sasa.”PICHA|MAKTABA
Hatua ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kususia vikao vya Bunge hilo imezua hofu kwamba inaweza kukwamisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya hasa katika kufanya uamuzi wa kupitisha ibara za Katiba hiyo.
Wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), juzi walitoka nje na kususia vikao vya Bunge hilo kwa madai kwamba hawaridhishwi jinsi mambo yanavyokwenda.
Kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo za 2014, zinasema ili ibara au Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote za Muungano.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kanuni ya 37 (1), inasomeka: “… ili ibara au rasimu iweze kupitishwa, itahitaji kuungwa mkono na wingi wa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar.”
Taarifa zisizo rasmi zinasema awali ili kuwezesha kupatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Zanzibar, CCM kilikuwa kinakihitaji kupata kura 16 ikilinganishwa na idadi ya wajumbe wanaokiunga mkono.
Kwa maana hiyo kuondoka kwa wanachama wa Ukawa kunamaanisha kwamba Bunge Maalumu haliwezi kupata akidi inayotakiwa wakati wa kufanya uamuzi wa kupitisha ibara kwa mujibu wa kanuni hizo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema jana kuwa hawatarejea katika Bunge hilo hadi kutakapokuwa na maridhiano ambayo kwa upande wao ni kuzingatiwa kwa rasimu iliyotokana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hivi sasa si vyema kutabiri kama wajumbe wa Ukawa watarejea bungeni au la.
“Mimi na wewe hatuwezi kutabiri, maana hawa ni viongozi wa kisiasa, wanaweza kuondoka leo, lakini kesho wakawa na mazungumzo na wenzao halafu wakarejea bungeni na shughuli zikaendelea,” alisema Hamad na kuongeza:
“Ni kweli kwamba kutokuwapo kwao kunaweza kuwa na athari katika kufanya uamuzi, lakini pia hatuwezi kusema ni athari zipi kwa sasa kwa sababu hakuna suala ambalo linapaswa kufanyiwa uamuzi kwa sasa.”
Hamad alisema kama alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta ipo fursa za kufanya mazungumzo na kwamba anaamini ikitumika vizuri, Bunge litaweza kuendelea na kufikia mwisho mwema.
“Kwa hiyo mimi nasema sisi tusubiri, maana hadi sasa hatujapata kufahamu kama kuondoka kwao watarejea baada ya Pasaka, Jumanne ijayo au ndiyo wameondoka moja kwa moja au ni vipi, ndiyo maana nasema ni vigumu kudhania kitakachotokea,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Wasusia Kamati ya Uongozi
Jana, wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo ambao ni wanachama wa Ukawa walisusia kikao hicho licha ya kualikwa na Sitta, ikiwa ni hatua ya kuendeleza mgomo dhidi ya mambo yote yanayohusu Bunge Maalumu.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alisema juzi kuwa alipata taarifa ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge la Muungano, lakini alipofika katika ukumbi husika alikutana na Kamati ya uongozi ya Bunge Maalumu na kuondoka.
“Nilipofika huko nikakuta kikao kilichokaa katika ukumbi huo ni cha Bunge Maalumu la Katiba, katika mazingira hayo nilikataa kushiriki, nikaondoka,” alisema Mbowe.
Baadhi ya wajumbe Bunge hilo waliohojiwa jana wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, walisema haitawezekana kupata theluthi mbili ya kura hasa upande wa Zanzibar, katika kupitisha rasimu.
Mjumbe kutoka kundi la 201, Maria Sarungi alipoulizwa jana alisema: “Nasikia kwamba kwa hesabu walizonazo Ukawa na CCM wenyewe hiyo theluthi mbili haiwezekani.”
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Pandu Ameir Kificho alipoulizwa jana kuhusu hofu hiyo, alisita kutoa maoni yake akisema hana uhakika kama Ukawa watarudi bungeni au la... “Sielewi kitakachoendelea kama hawatarudi... huenda baada ya kupata maoni ya wananchi huko nje wakaamua kurudi.”
Mwenyekiti wa chama cha APPT- Maendeleo, Peter Mziray alisema kama Ukawa hawatarudi katika meza ya mazungumzo, hakuna jinsi, lazima Katiba ya 1977 itaendelea kutumika.
Taarifa ya nyongeza na Sharon Sauwa na Ibrahim Bakari