Quantcast
Channel: PAMOJA BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

DK. SLAA, MBOWE WAPIGWA MARUFUKU MWANZA

$
0
0
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, wamepigwa marufuku kukanyaga jijini Mwanza.



Pamoja na onyo hilo, pia viongozi hao wametakiwa kufanya kila wanaloweza ili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na wenzake waliovuliwa madaraka, warudishwe madarakani ndani ya siku nne kuanzia jana.

Kauli hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa Vijana Kanda ya Magharibi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Matawi ya CHADEMA, Mkoa wa Mwanza, Robert Gwanchele, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Gwanchele, yeye na wenzake wamelazimika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa wanapinga kitendo cha kuvuliwa madaraka kwa viongozi hao kwa kuwa kilifanyika kinyume cha Katiba ya chama hicho.


“Pamoja na kuwapiga marufuku kukanyaga mkoani Mwanza viongozi hao wa kitaifa, kama Zitto, Dk. Mkumbo Kitila pamoja na Samson Mwigamba wasiporejeshwa madarakani, hadi Desemba 4 mwaka huu, vijana Kanda ya Magharibi tutaandaa maandamano yasiyo na ukomo kushinikiza Dk. Slaa na Mbowe wajiuzuru ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.


“Chadema tumeingiliwa na mdudu aitwae ubinafsi kwani kuna baadhi ya viongozi wa chama ni makuwadi wa viongozi wetu wa ngazi za juu kufanya wanayotaka bila kuchukuliwa hatua.

“Chadema ni chama kinachojali watu wa upande fulani wa nchi, hivi viongozi kama Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) pamoja na Kileo ambao waliamua kumshambulia Zitto kupitia mitandao ya kijamii wamechukuliwa hatua gani na chama?.

“Tutahakikisha tunawaondoa viongozi wote wa ngazi za juu kwa nguvu ya umma kwani Chadema sio mali ya mtu binafsi, chama hiki nicha wanachama.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Hatutaki kuyumbishwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi, hao wanapaswa kukaa pembeni kwanza kupisha uchunguzi na kama hawataki kupisha nguvu ya umma itawaondoa na ndio maana sisi vijana wa Kanda ya Magharibi, tumeamua kuwapiga marufuku Mbowe na Dk. Slaa wasikanyage Mwanza kwani wao tayari wameamua kujijengea himaya yao isiyoguswa katika mikoa ya kaskazini, sasa Mwanza wanakuja kutafuta nini.

“Mbowe na Dk. Slaa ni watuhumiwa hawapaswi kuendelea kuwa viongozi wa Chadema, hao wanapaswa kujiondoa ili nao wachunguzwe juu ya matumizi mabaya ya fedha za chama,” alisema Gwanchele.

Pamoja na kuwashambulia Mbowe na Dk. Slaa, Gwanchele pia aliwarushia kombora wabunge wa Chadema wanaotoka Mkoa wa Mwanza kwa kile alichosema nao wameshiriki katika kuvuliwa madaraka kwa Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba.

Kutokana na hali hiyo, alisema wabunge hao, Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Salvatory Machemli (Ukerewe), wamepoteza uhalali wa kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Mwanza.

“Wabunge wa chadema Mkoa wa Mwanza hivi sasa wanajiona wako juu ya chama na wamekuwa wakitoa matamko ya kuunga mkono kuondolewa kwa Zitto na wenzake wakati sisi wananchi hatukuwatuma kufanya hayo.

“Kwa hiyo, nao wanapaswa kuondolewa madarakani mara moja kwa usaliti wao kwa wapiga kura wao,”alisema.


BAVICHA Arusha

Wakati Mwanza wakisema hayo, Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Mkoa wa Arusha, limewataka Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba, kuacha tabia ya kulalamika mitaani, badala yake wawasilishe malalamiko yao ngazi husika.

Akizungumza na Rai Jumatatu jijini hapa jana, Mwenyekiti wa BAVICHA, Mkoa wa Arusha, Efatha Nanyaro, alisema uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao, ulikuwa sahihi.

“Kwanza sisi tunaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu japokuwa tangu viongozi hao wavuliwe uongozi, kumekuwa na malalamiko na taarifa nyingi za upotoshaji.

“Tunawaambia wasilalamike mitaani bali wapeleke malalamiko yao Baraza Kuu au wasubiri mkutano mkuu kuliko kulalamika pembeni.

“Pamoja na hayo, naamini kama watapeleka malalamiko yao mbele ya Baraza Kuu, bado siamini kama kikao hicho kinaweza kuja na uamuzi tofauti na ule uliotolewa na Kamati Kuu wa kuwavua uongozi,” alisema Nanyaro.

Nanyaro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Levolosi, alisema taasisi yoyote inayoogopa kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wake wanaokiuka taratibu zilizowekwa, itakuwa taasisi dhaifu na haifai kuwapo. 

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, amesema chama hicho hakiwezi kufa hata kama aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe, atakihama.

Dk. Slaa ametoa kauli hiyo wakati Zitto ameshaweka wazi, kwamba hana mpango wa kukihama chama hicho na kwamba wanaotaka akihame, wamuondoe wao. 

Zitto alitoa msimamo huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Katika mazungumzo yake na Rai Jumatatu yaliyofanyika juzi, Dk. Slaa alisema Chadema ni taasisi yenye watu wengi na hivyo hakiwezi kuathirika kwa namna yoyote ile hata kikiondokewa na kiongozi maarufu.

Dk. Slaa aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza kwa simu na Rai Jumatatu.

“Chadema ni ya Watanzania, hivi Dk. Slaa akifa leo Chadema itakufa?, sasa chama kitaathirika vipi kwa kuondokewa na mtu mmoja wakati kuna mamilioni ya Watanzania wanaokimiliki kuanzia kwenye misingi ya chini?.

“Watanzania wanachopigania ni ukombozi wao, Chadema ndiyo mkombozi wao,” alisema Dk. Slaa kwa kifupi.

Kuhusu mashitaka 11 yanayowakabili Zitto, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema barua hizo zilishatoka kwake hivyo hawezi kuzisemea na wenye mamlaka ya kuyasema mashitaka hayo ni wao wenyewe.

Akizungumzia kuhusu Zitto kujitetea mbele ya Kamati Kuu kabla ya kuvuliwa nyadhifa zake, kuhusiana na waraka anaotuhumiwa kuuandaa, alisema ni suala la ndani ya vikao vya chama.

“Alikuwepo kwenye kikao, lakini mambo mengine ya kikao ni mambo ya ndani, Katibu Mkuu ni Katibu wa vikao na Chadema anazungumzia taifa, hazungumzii mtu mmoja mmoja.

“Kuhusu huo waraka, mimi nina nyaraka nzito sana huo waraka mnaouona wa maana ni takataka tu, na ninaona upuuzi kushughulikia mambo ya kipuuzi kama hayo,” alisema Dk. Slaa.

RAI

Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>