Picha za Katie Gee kabla (kushoto) na baada ya kushambuliwa na tindikali Zanzibar. PICHA | AFP
Dar es Salaam. Familia ya Waingereza, Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18, waliomwagiwa tindikali huko Zanzibar, wameiomba Serikali ya Uingereza kuishinikiza Tanzania kuharakisha kuwawajibisha waliohusika na tukio hilo.
Waingereza hao ambao walikuwa walimu wa kujitolea katika shule ya St Monica, Tomondo, Zanzibar, walimwagiwa tindikali na watu wawili wasiojulikana wakati walipokuwa kwenye matembezi ya jioni katika eneo la Mji Mkongwe Agosti 7, mwaka huu.
Baada ya tukio hilo lililowajeruhi kiasi kikubwa katika maeneo ya kifua na mikononi, walipewa matibabu katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, kisha wakarudishwa kwao kwa matibabu zaidi.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alipowatembea wasichana hao hospitalini, Rais Jakaya Kikwete alisema tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa habari wa Polisi wa Kimataifa (Interpol) Kanda ya Tanzania, inaeleza kuwa familia ya wasichana hao hairidhishwi na namna Serikali ya Tanzania inavyolishughulikia suala hilo kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuwatambua wahusika.
Mtandao huo umemnukuu baba yake Trup, Marc alipokuwa akizungumza na Redio 4 ya BBC, kuwa kuna wingu zito lililotanda kuhusu kesi hiyo, kwa kuwa hadi sasa Serikali ya Zanzibar imeshindwa kuonyesha picha za wahusika ili zitambuliwe na wasichana hao, ingawa imekwisha kuwahoji watu kadhaa.
“Picha haziwezi kutumwa katika muundo bora unaokubaliwa na Interpol au Mamlaka za Uingereza, kutokana na sababu hizo hakuna hata mmoja ameshaziona hizo picha,” alisema Marc.
Naye baba mlezi wa Gee, Doug Morris, alisema: “Kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Jumuiya ya Madola wako makini kusaidia watu hao kufikishwa mbele ya sheria kwa niaba ya raia wa Uingereza, tulitegemea wafanye kila linalowezekana, lakini hakuna dalili zozote zinazoonekana za kutaka kuharakisha jambo hili.”
Aliongeza:“Kama wanamaanisha wanachokisema na ni muhimu kwao kuwatafuta waliotekeleza kitendo hicho ili wawafikishe kwenye vyombo vya sheria, basi watusaidie kwa kila njia ambayo wanaweza.
“Kila mtu ameanza kufikiri kuwa wanatuchezea, kila wiki tunakatishwa tamaa. Huu ni uharibifu ambao hauwezi kupita tu bila mtu kuadhibiwa kwa manufaa ya wasichana wale au mtu mwingine yeyote.
“Aina gani ya ujumbe unaoletwa, kwamba unaweza kufanya jambo baya halafu usifanywe kitu chochote?”
Alisema kuwa wangependa suala hilo lifike mwisho haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.
Familia hiyo inasema kuwa hadi sasa haijafahamu sababu ya wasichana hao kushambuliwa kwa tindikali, kwa kuwa muda wote walipokuwa Zanzibar walionyesha tabia njema na kuvaa mavazi ya heshima.
Mzazi huyo wa Trup aliongeza kuwa: “Ninadhani mamlaka za Tanzania haziyachukulii masuala ya mambo ya nje ya nchi kwa umakini unaotakiwa, tunataka ifanye kazi.
“Wasichana wanataka kujua kama tukio lile lilitokana na rangi yao au dini kwasababu hawajui ni kwa nini lilitokea.”
Akizungumzia maendeleo ya afya ya binti yake, alisema kuwa Kirstie anaendelea vizuri na kwamba amesharudi chuoni kuendelea na masomo yake, ingawa bado anakwenda hospitali kupata matibabu.
“Anavaa vazi maalumu la kufunika makovu aliyoyapata, atafanya hivyo saa 23 kwa mwaka mzima. Ingawa anaendelea vizuri kimwili na kiakili, bado anapita katika kipindi kigumu,” alisema.
Akielezea maendeleo ya kiafya ya Katie, Morris alisema kuwa naye anaendelea na matibabu na kwamba hali yake inaendelea kuimarika.
Danadana za Polisi
Alipoulizwa maendeleo ya kesi hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kuwa jalada la tukio hilo lipo Zanzibar, hivyo mwandishi awasiliane na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kupata ufafanuzi.
Hata hivyo, alipopigiwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa simu zake zote mbili ziliita bila kupokewa. Alipotafutwa Ofisa Habari Mkuu Jeshi la Polisi Zanzibar, INSP Mohammed Mhina alisema kuwa kuna kesi nyingi za matukio ya watu kumwagiwa tindikali yaliyotokea Zanzibar ambayo yatatolewa ufafanuzi yote kwa wakati mmoja.
“Matukio ya kumwagiwa tindikali yapo mengi, hata hilo unalolizungumzia ninalikumbuka, ni vyema hayo yote yakazungumzwa kwa wakati mmoja,” alisema na kuongeza kuwa apigiwe simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, kwa kuwa ndiye anayelijua vizuri jambo hilo.
Kwa upande wake, Mkadam alisema suala hilo halipo tena mikononi mwake kwa kuwa lilishapelekwa kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Mwananchi lilimtafuta Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yusuf Ilembo, lakini simu zake ziliita bila majibu.
Kauli ya Dk Shein
Akihutubia Baraza la Idd Fitr mwaka huu mjini Zanzibar, Rais wa visiwa hivyo, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali yake itahakikisha inawasaka na kuwafikisha mahakamani waliopanga na kufanya shambulio hilo.