Mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa nchini Cameroon 2019, kati ya Taifa Stars dhidi ya Lesotho uliokua uchezwe jumamosi saa 2 usiku Uwanja Taifa, umehamishiwa uwanjawa Azam Complex Chamazi.
Akithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema mchezo huo utachezwa Azam Complex Chamazi.
Taifa Stars itaondoka leo kuelekea Alexandria Misri kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mechi ya Afcon vs Lesotho tar 10/06— Jamal Malinzi (@jamalmalinzi) May 30, 2017
Taifa Stars iliyoweka kambi ya wiki moja nchini Misri, imelazimika kubadilisha uwanja wa kuchezea kutokana na mkandarasi wa uwanja wa Taifa kung’oa nyasi zote kwa ajili ya matengenezo .
Kutokana na matengenezo hayo kumeipelekea Taifa Stars kucheza mechi yake dhidi ya Lesotho kwenye uwanja wa Azam Complex, kwa kuwa ndiyo uwanja pekee Tanzania uliokaguliwa na kupitishwa kutumika kwa michuano ya Kimataifa sanjari na Uwanja wa Taifa.
Ukarabati wa uwanja wa taifa umetokana na ukarabati unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na waandaaji wa ujio wa ziara ya klabu ya Everton mapema mwezi ujao.
Tangu ufungukiwe rasmi 2008, Uwanja wa Taifa ulikuwa haujawahi kufanyiwa marekebisho ya sehemu ya kuchezea, na wataalamu wa ufundi wa klabu ya Everton walisema nyasi za uwanja huo zimechakaa zinapaswa kubadilishwa ili kuendana na hadhi ya ujio wa klabu hiyo.
Ziara ya klabu ya Everton Tanzania inaratibiwa na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa inayowadhamini miamba hao wa Uingereza, na klabu za Simba, Singida United na Yanga zote za Tanzania.