Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kusimamia na kufuatilia sheria na miongozo yote iliyotolewa ili kuhakikisha lengo la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ikiwemo safari za nje na posho za wajumbe wa Bodi za mashirika na Taasisi zote za Umma linafanikiwa.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa (CCM), Mhe. Japhet Hasunga ambaye alitaka kujua hatua ambazo Serikali inatarajia kuchukua kudhibiti matumizi ya fedha za Umma katika Taasisi zake.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu kupitia Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge ikiwemo Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 ambayo imebainishwa hatua mbalimbali za kibajeti zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma katika Mashirika na Taasisi za Umma.
“Sheria hiyo imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mipango na Bajeti wa Serikali unaojumuisha Mashirika na Taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbalimbali ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika,” alifafanua Dkt. Kijaji
Alisema kuwa kupitia Sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia bajeti za Mashirika na Taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na mipango ya Serikali inayotarajiwa kutekelezwa.
Mhe. Kijaji alibainisha kuwa katika Sheria hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu la kupitia na kuridhia kanuni za fedha za Mashirika na Taasisi zote za Umma ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma.
“Sheria nyingine iliyopitishwa na Bunge ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 ambayo iliweka ukomo kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara,” aliongeza Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa katika kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa Hazina inatekeleza majukumu yake kisheria, imetoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti matumizi ya Mashirika na Taasisi za Umma ili kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
“Miongoni mwa miongozo hiyo ni barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015 ya kudhibiti safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa watumishi wa Mashirika na Taasisi za Umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu kubwa ya fedha za Umma,” alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa waraka wa Msajili wa Hazina Na. 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma pia ni miongoni mwa miongozo ya kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwani waraka huo umefuta posho za vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne kwa mwaka.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma ulikuwa na lengo la kuendeleza jitihada za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za Umma.
Alisema kuwa Waraka huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa bado Serikali itaendelea kuhakikisha matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu.