Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mbuzi Mugumu Serengeti ikiwa sehemu ya kukamilisha ziara yake ambapo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa Serengeti na kuwapongeza kwa kutunza mazingira. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Serengeti inayojengwa makao makuu ya wilaya Mugumu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia mfano wa majengo ya hospitali ya wilaya ya Serengeti inayojengwa makao makuu ya wilaya Mugumu kulia ni Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Kisaka.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa wilaya ya Serengeti na wa mkoa Mara kukamilisha haraka awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri kwenda mikoa ya jirani ya Arusha na Mwanza kwenda kupata huduma afya.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo leo 6-June-2017 kwenye mkutano wa hadhara mjini Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara mara baada ya kutembelea ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya na kuweka jiwe la msingi.
Makamu wa Rais amesema kutokana na wilaya ya Serengeti kupata wegeni wengi kutoka nje ya nchi ambao wanaenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo ni muhimu kwa viongozi wa wilaya na mkoa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kukamilisha ujenzi huo haraka ili wananchi waweze kupata huduma za afya za uhakika katika wilaya yao.
Makamu wa Rais amesema kukamilika kwa ujenzi huo wa awamu ya kwanza kutaondoa taabu kubwa wanayopata wananchi wa wilaya ya Serengeti katika kupata huduma ya afya karibu na maeneo yao.
Katika kuunga mkono jitihada hizo za ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Serengeti, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni Tano na amewaahidi wananchi wa wilaya ya Serengeti kuwa atakikisha fedha kutoka Serikalini ambazo zinatakiwa kupelekwa wilayani humo zinapelekwa haraka ili kukamilisha ujenzi huo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewataka wananchi kote nchini kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na rushwa na ufisadi ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na manufaa kwa wananchi wote.
Amewaomba wananchi nchini wasirudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa bali waendelee kubaini watu wanaofanya vitendo hivyo ili Serikali iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria .
Kuhusu tatizo la mimba mkoani Mara, Makamu wa Rais ameonyesha kuchukizwa na vitendo hivyo na kuomba vyombo vya dola na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kukomesha mimba za utotoni mkoani Mara.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mara Dkt Charles Mlingwa amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa maelekezo yote anayoyatoa katika ziara yake yatafanyiwa kazi ipasavyo ili kuondoa kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mara ameomba wananchi wa Mkoa wa Mara kuwepa pembeni tofauti zao za kisiasa bali washirikiane na Serikali katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan bado anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mara ambapo hapo kesho atafanya ziara katika wilaya za Butiama na Musoma mkoani Mara.