Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka shda la maua kwenye Mnara wa kumbukumbu ya ajali ya ndege ya kivita iliyotokea mwaka 1978 kwenye Msitu wa Muhunda ,wilayani Butiama mkoani Mara. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akutana na Mama Maria Nyerere nyumbani kwa Mama Maria Butiama leo mara baada ya kuhutubia kwenye kilele cha siku ya mazingira Duniani.Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipanda mti kwenye Msitu wa asili ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye kilele cha siku ya mazingira duniani ambapo kitaifa imeadhimishwa Butiama.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimwagia maji mti alioupanda kwenye Msitu wa asili ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye kilele cha siku ya mazingira duniani ambapo kitaifa meadhimishwa Butiama. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wananchi kijijini Butiama mkoani Mara wakati wa kilele cha siku ya mazingira Duniani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia kiatu cha kusaidia walemavu wakati alipotembelea banda la Kituo cha Walemavu cha Ziwa Victoria (Lake Victoria Disability Centre) kinachoshughulika na kutengeneza viungo bandia kwa watu wenye ulemavu kabla ya kuhutubia kwenye kilele cha siku ya mazingira duniani ambapo kilele chake kimefanyika kwenye viwanja vya Mwenge,Butiama
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia namna samaki anaweza kufugwa vizuri bila kuharibu mazingira na kuleta manufaa kabla ya kuhutubia kwenye kilele cha siku ya mazingira duniani ambapo kilele chake kimefanyika kwenye viwanja vya Mwenge,Butiama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa viwanda na migodi ambayo inafanya shughuli zake za uzalishaji kwa kuharibu mazingira ikiwemo utitirishaji wa kemikali kwa wananchi kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa wananchi na viumbe hai wengine.
Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo tarehe 4-Jun-2017 kijijini Butiama mkoani Mara wakati anahutubia wananchi katika kilele cha siku ya mazingira Duniani.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema uharibifu wa mazingira ukiachiwa uendee nchini ni hatari kwa usalama wa maisha na viumbe hivyo ni muhimu kwa viongozi katika ngazi zote kuchukua hatua zitakazosaidia kukabiliana na vitendo hivyo kote nchini.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kwa ushirikiano na jamii kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuokoa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuai, kudhibiti uchomaji miti kiholela ili kurejesha uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu katika maeneo mengi nchini.
“Kutozingatia hifadhi ya mazingira kunaweza kusababisha kuparaganyika kwa mfumo huo na kufanya maisha yetu na ya vizazi vijavyo kuwa mashakani”. Amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema katika kuadhimisha siku ya mazingira Dunia viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kuelimisha wananchi na kuwahamasisha ili kila mtu ashiriki katika juhudi za kuwa na uchumi unaozingatia hifadhi ya mazingira.
Kuhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa nchini, Makamu wa Rais aipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuruhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa bila kiingilio na kusema mpango huo ni mzuri na unatakiwa kufanyika kila mwaka.
Amesema kuwa mkakati huo unalenga kuhamasisha wananchi ili kuwa mahusiano rafiki na mazingira kwa kuzingatia ukweli kwamba jinsi wananchi wanapoona ndipo wanapoamini na kuelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Ameeleza kuwa katika kuadhimisha siku hiyo inapasa jamii kutafakari mchango wa kila sekta na kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira January Makamba amesema Serikali imeamua kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kijijini Butiama kama hatua ya kuenzi mchango mkubwa uliofanya na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika uhifadhi wa mazingira.
Amesema baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere alifanya kwa vitendo katika kuhifadhi mazingira ambapo alianzisha msitu wake katika eneo la Butiama hivyo wananchi wote ni lazima waige mfano huo katika kulinda na kutunza mazingira.
Kwa upande wa familia na mwalimu Nyerere wameishukuru Serikali kwa kupeleka maadhimisho hayo kijijini Butiama ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua mchango wa baba wa taifa katika uhifadhi wa mazingira nchini.
Kabla ya Kuhutubia katika Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alipanda miti katika msitu wa Mwalimu Nyerere na kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya ajali ya Ndege ya Kivita ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliopo katika msitu wa Muhunda katika kijiji cha Butiama mkoani MARA.