Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu kabla ya ufunguzi wa Semina kwa wastaafu watarajiwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Semina kwa wastaafu watarajiwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza
Baadhi ya washiriki wa Semina ya Wastaafu Watarajiwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa Semina ya Wastaafu Watarajiwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu Mwanza.
Baadhi ya Wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina kwa Wastaafu Watarajiwa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akionyesha Vitabu vya PSPF kwenye kutoa elimu kwa Wanachama wa mfuko huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza waajira wasiopeleka au kuchelewesha michango ya wanachama kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii nchini wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo 3-June-2017 Jijini Mwanza wakati anafungua semina ya maisha baada ya kustaafu,fursa ya mafao,uwekezaji iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kwa ajili ya wastaafu watarajiwa 450 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa waajiri wakichangia kwa mujibu wa sheria kwenye mifuko hiyo watawezesha wanachama wao kupata mafao kikamilifu na kwa wakati.
Kuhusu madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini, Makamu wa Rais amewahakikishia Wakurugenzi wa mifuko hiyo kuwa Serikali inashughulikia madeni hayo na baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa madeni hayo basi malipo yatafanyika haraka iwezekanavyo.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha michango ya pensheni kwa wafanyakazi wa taasisi zinazopata ruzuku kutoka Serikalini inalipwa kwenye mifuko hiyo kwa wakati.
Aidha, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza wastaafu watarajiwa kote nchini waache tabia ya kukata tamaa baada ya kustaafu bali wajipange vyema na kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo, kilimo na biashara.
Amesema kuwa kama wastaafu hao watawekeza katika maeneo hayo watatoa ajira kubwa kwa vijana badala ya kutumia mafao yao kwenye matumizi yasiyo ya lazima.
“Wazee ni rasilimali na hazina kubwa kwa taifa kama waswahili wasemavyo panapo wazee hapaharibiki jambo hivyo basi ni matumaini yangu kuwa mfuko wa PSPF mtaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu kuhakikisha kuwa hazina hii ya wazee wetu wanapata haki zao kwa mujihu wa sheria za nchi pale wanapohitaji huduma toka kwenu.”Amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameonya wastaafu hao watarajiwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima bali watumie fedha watakazopata katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya maslahi yao ya baadaye.
Makamu wa Rais pia amepongeza jitihada zinazofanywa na mfuko wa PSPF kwa kutoa mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa ajili ya kuwasaidia kujipanga vyema pindi watakapostaafu utumishi wao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amewahakikishia wastaafu hao watarajiwa kuwa wa mkoa wa Mwanza kuwa Serikali itaendelea kusimamia vyema mifuko ya hifadhi ya jamii ili iweze kutoa mafao bora na kwa wakati.
Dkt Ashatu Kijaji pia amehimiza wastaafu hao watarajiwa kutumia vizuri mafao wanayopata kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.