Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula akiwasilisha mada inayohusu Sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 wakati wa mafunzo kwa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini yaliyofanyika leo mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuifahamu Sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
Meneja wa Idara ya Mbinu za kitakwimu, Viwango na Uratibu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Emilian Karugendo akitoa ufafanuzi wa namna Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyokusanya takwimu rasmi nchini kwa kuzingatia kanuni za kitaifa na kimataifa wakati wa mafunzo kwa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini yaliyofanyika leo mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuifahamu Sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
Baadhi ya Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati wa mafunzo kwa Maafisa hao yaliyofanyika leo mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuifahamu Sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
Baadhi ya Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati wa mafunzo kwa Maafisa hao yaliyofanyika leo mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuifahamu Sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.
Na: Emmanuel Ghula
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa mafunzo kwa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini leo mkoani Morogoro kuhusu Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 ili kuwajengea uwezo wa kufahamu namna sheria hiyo inavyofanya kazi.
Akifafanua sheria hiyo, Mwanasheria wa NBS, Oscar Mangula amesema sheria ya Takwimu No. 9 ya mwaka 2015 imeipa Ofisi ya Taifa ya Takwimu jukumu la kuratibu na kusimamia ukusanyaji wa takwimu rasmi nchini.
“Sheria ya Takwimu No. 9 ya mwaka 2015 ni sheria inayoipa NBS jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli zote za upatikanaji wa takwimu rasmi nchini. Hivyo, kama taasisi yoyote inataka kufanya utafiti kwa minajili ya kutoa takwimu rasmi ni lazima iwasiliane na NBS ili kupata miongozo ya ukusanyaji wa takwimu rasmi,” amesema Mangula.
Mangula amesema kuwa, ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ama taasisi kuendesha utafiti na kuchapisha au kutoa takwimu rasmi bila kuwasiliana na NBS kwani inaweza kukusanya takwimu ambazo hazina ubora na zinazoweza kupotosha umma.
Aidha, Meneja wa Takwimu za Kodi kutoka NBS Fred Matola amesema NBS hutoa takwimu rasmi kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa inayotolewa na Umoja wa Mataifa ili kukidhi mahitaji ya nchi pamoja na kutumika kimataifa.
“Takwimu rasmi zinakusanywa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na umoja wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya nchi, hivyo NBS ina wajibu kisheria kusimamia upatikanaji wa takwimu rasmi nchini”, amesisitiza Matola.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kuratibu na kusimamia ukusanyaji, uchambuzi na upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.