Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Rhoda Kunchela aliwasilisha bungeni furushi la risiti za mwenge wanazodaiwa kuchangishwa kwa nguvu, walimu na wafanyabiashara.
Mbunge Kunchela aliomba kutoa hoja ili ijadiliwa na Bunge kuhusiana na kile alichodai walimu, wafanyabiashara na wafanyakazi kuchangishwa kwa nguvu michango ya mwenge.
“Mkononi hapa nina risiti zaidi ya 300 za michango inayochangishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali wakiwepo walimu, wafanyabiashara na wafanyakazi wa kada mbalimbali,”alisema.
“Ni malalamiko ya muda mrefu sana kwamba wamekuwa wakilazimishwa michango hii, kibaya zaidi Serikali iliwahi kutoa taarifa hapa bungeni kuwa michango hii ni hiyari,”alisisitiza Kunchela.
“Tulipofikia sasa hivi si sawa kwa mikoa mbalimbali kuendelea kulazimishwa kuchangia mwenge wa uhuru wakati ni hiyari. Jambo hili Serikali itoe tamko au Bunge lako lijadili suala hili,” alisema.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alikataa kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe lakini akamtaka mbunge huyo kukabidhi risiti hizo kwa Bunge ili nalo lizikabidhi serikalini kwa hatua zaidi.
“Ningependa hayo marisiti yako, hilo furushi la risiti, tupewe tutaikabidhi Serikali tuone,”alisema Chenge na kuwaagiza wafanyakazi wa Bunge waliokuwa ndani ya ukumbi kwenda kuzichukua.
Chanzo: Mwananchi