Na Regina Mkonde
Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amefunguka kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo, ukimya wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, muenendo wa shughuli za Bunge pamoja na tukio lililotokea hivi karibuni la Askari Polisi mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua risasi hewani mbele ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima baada ya kutokea majibizano yaliyosababishwa na dereva wa Malima kuegesha gari vibaya.
Nape amefunguka hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari ambapo alisema, Kinana ambaye baadhi ya watu wanadai kuwa ukimya wake umetokana na kujiuzulu, yuko katika wadhifa wake wa ukatibu mkuu na anaendelea kufanya kazi za chama.
“Mimi sio msemaji wa chama, lakini Katibu Mkuu yupo na anafanya kazi yake kama kawaida…., mimi bado ni mwanachama na muumini mzuri wa CCM inayopenda haki, na nina amini hiki ndicho chama pekee bora kitakachoweza kuwakomboa watanzania pamoja na kuamiwa ikiwa kitatekeleza mkataba wake na wananchi ambao ni wa kutimiza ahadi zake ilizo ziahidi,” alisema.
Kuhusu tukio la Askari Polisi kufyatua risasi hewani, ambalo Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro alisema ulikuwa uamuzi wa busara wa kuondoa taharuki katika tukio hilo, na mbinu ya kuwatia nguvuni watuhumiwa.
Nape alishauri vyombo vya dola kutotumia nguvu kwani kitendo hicho kitajenga hofu na chuki baina ya serikali na wananchi na hata kwa chama tawala CCM, huku akiisihi serikali kuondoa vitendo vinavyotia hofu wananchi.
“Ni vizuri vyombo vya dola vikatimiza majukumu yake kwa kuwa ni vyombo vya wananchi, si vizuri vikitumia nguvu kubwa pale isipostahili. Ifikie hatua raia asiye na silaha Polisi wasitumie nguvu kushughulika naye kwa kutumia silaha. Nimeona ile video ikionyesha Malima alikuwa anauliza chanzo cha tatizo,” alisema na kuongeza.
“Kuna nchi tamaduni zake ni kutumia mabavu na nyingine zinatumia demokrasia, nchi yetu utamaduni wake si wa kutumia nguvu, tumezoea kuelewana kwa mazungumzo. Vyombo vya dola visitumie nguvu kwa kuwa tunajenga usugu usio na maana. Na kama kuna mazingira hatarishi basi nguvu itumike.”
Kuhusu mienendo ya shughuli za Wabunge Bungeni, aliwataka wabunge kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwawakilisha na kusimamia vema masilahi ya wananchi wanaowawakilisha, pamoja na kuisimamia serikali kutekeleza vizuri majukumu yake.
“Bunge ni mkutano wa wananchi, na wabunge wapo kwa niaba ya wananchi katika kupitisha na kushauri mipango ya serikali. Ni vizuri wasimame katika maeneo yao, wasiwe wapiga makofi, pale serikali inapofanya vizuri ipongezwe na inapofanya vibaya ikosolewe,” alisema.
Kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari, alisema ifikie hatua wananasiasa wawe na ngozi ngumu ya kuvumilia kukosolewa na watu kupitia vyombo vya habari. Pia ameshauri wananchi wanaotaka maonesho ya vikao vya bunge moja kwa moja, kuuomba mhimili huo kubadilisha sheria zake ambazo zimeipa mamlaka ya kuamua namna ya kuendesha shughuli zake.
“Naamini uamuzi wa siku ile wa kuzuia shughuli za bunge live ulikuwa sahihi sababu sheria zinasema Bunge litaendeshwa kwa sheria zake. Wananchi wanaozungumzia Bunge live, waliombe libadilishe sheria zake ili lianze kuonyeshwa live,” alisema