Tarehe 15 ya mwezi huu wa Mei kila mwaka, Wapalestina kote duniani wanaadhimisha kumbukumbu ya kutokea janga(NAKBA) kubwa la kibinadamu la kukaliwa kwa mabavu ardhi yao, huku wenyewe wakifukuzwa na kulazimika kuyaacha makazi yao, kulikofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israeli, ambapo mwaka huu wa 2017 ni maadhimisho ya miaka 69, tangu kutokea kwa janga hilo. Siku hii inajulikana kama siku ya Nakba au siku ya nakama,janga,maafa na msiba mkubwa kwa wananchi wa Palestina wasio na hatia.
Ripoti iliyotolewa na Kamati Kuu ya Kitaifa ya kumbukumbu za Siku ya Nakba imeeleza kuwa, haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi yao ya asili haipingiki wala haina mbadala. Aidha tarehe 15 Mei kila mwaka, Wapalestina duniani kote hufanya maandamano kukumbuka Siku ya Nakba, ambayo inakumbusha masaibu ya kufukuzwa kwa nguvu kwa maelfu ya Wapalestina kutoka katika ardhi yao ya asili, kulikofanywa na vikosi hivyo dhalimu vya Wazayuni wa Israeli mwaka 1948. Wazayuni pia walifuta ramani za miji na vijiji zaidi ya 500 vya Wapalestina na kusababisha Wapalestina wanaokadiriwa mamilioni kuwa wakimbizi kwa karne kadhaa kwenye nchi jirani za kiarabu.
SIKU YA NAKBA:
Hivyo basi, Mei 15 kila mwaka Wapalestina duniani kote huadhimisha siku hiyo ya Nakba, inayowakumbusha dhuluma ya kihistoria iliyowapata,ambayo masaibu yake yanaendelea kuwanyima raha hadi leo hii. Waliihama ardhi yao kilazima, ikiwa ni matokeo ya uhalifu wa wanamgambo dhalimu wa Israeli dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina mwaka 1948.
Kufukuzwa huko kwa Wapalestina toka katika ardhi yao ya asili, kumekuwa kunajulikana kama Al Nakba (Maafa), huku zaidi ya Wapalestina laki nane (800,000) wakiwemo wanaume, wanawake, na watoto, wakilazimishwa kuyahama makazi yao kufuatia tamko la kuundwa kwa Israeli mwaka 1948,litokanalo na kile kilichojulikana kama harakati za kizayuni.
Wapalestina walikimbilia katika maeneo mengine ya Palestina ambayo yalibakia katika udhibiti wa ndugu zao wa kipalestina na Waarabu au nchi jirani za Kiarabu, huku wakiacha kila kitu zikiwemo mali, biashara, na akiba yao ya vyakula zikiwemo nafaka. Mara baada ya kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka katika nchi yao, mfululizo wa sheria za kidhalimu zilipitishwa na serikali ya Israeli, zinazolenga kuzuia wakimbizi wa Kipalestina kutoka na kurudi majumbani mwao.
Kufukuzwa kwa wapalestina kutoka katika ardhi yao ya asili,haikuwa tu ni dhuluma bali kumelenga pia kuwafutia uwepo wao,hadhi na kuwaondoa kabisa katika historia. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1948, theluthi mbili ya Wapalestina ilikuwa imefukuzwa kutoka katika nchi yao, kufuatia shambulio la kijeshi la Israeli.
Hali iliyopelekea kukimbia mauaji yaliyofanywa na wanamgambo wa kiyahudi katika maeneo mbalimbali ya Palestina, kama vile “Deir Yassin” na “Tantura”. Kiuhalisia vikosi hivyo vya kiyahudi vilipunguza idadi ya wapalestina kwa kuteketeza vijiji na miji zaidi ya mia tano (500).
Hivyo, kila mwaka ifikapo siku ya Nakba, Wapalestina hukumbuka na kuomboleza vitendo hivyo vya ugaidi wa Israeli uliotekelezwa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia zaidi ya laki nane (800,000). Idadi hiyo kubwa, wengi wao hawakuwa na uwezo wa kujitetea, kwani ni wale waliotokana na familia za wakulima wa kawaida wasio na silaha, ambao walikuwa wamefukuzwa kwa nguvu na kulazimika kuihama ardhi yao ya asili.
Serikali ya Israeli iliyoingia madarakani hivi karibuni, imepokonya ardhi ya wakimbizi wa kipalestina,bila kuheshimu haki zao au tamaa na matakwa yao ya kurudi nyumbani katika ardhi yao ya asili. Viongozi wa kiyahudi wametamka waziwazi kwamba, kuna haja ya kutumia nguvu za kijeshi ili kuwafukuza Wapalestina wengi vyovyote iwezekanavyo.
Kulikuwepo na mpango mkakati maalumu uliowekwa na wanamgambo wa kiyahudi ujulikanao kama “Haganah Militia’s Plan Dalet”,uliolenga kutekeleza uhalifu huo wa kuwafukuza kwa nguvu wapalestina kutoka katika ardhi yao,kwa mujibu wa kauli ya Waziri Mkuu wa kwanza wa Israeli David Ben Gurion. "Ni lazima kutumia njia mbalimbali zikiwemo ugaidi, mauaji, vitisho, kuwaondoa kwa ngvu na kukata huduma zote za kijamii ili kuwafukuzia mjini Galilaya, ambao ni mji wa mbali wa Kiarabu."
Mahali pengine duniani hali hii huchukuliwa kuwa ni uvamizi wa kutumia silaha, kufuatia kuporwa kwa ardhi ya wapalestina wasio na hatia,kwa kutumia silaha mbalimbali zikiwemo bunduki na mabomu dhidi ya familia zisizo na silaha.
Kuna wakimbizi wa kipalestina zaidi ya milioni saba (7) katika nchi jirani za Kiarabu na duniani kote hadi kufikia leo hii, ni ukweli usiopingika kwamba ndio idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani iliyobaki. Hadhi ya wakimbizi na haki zao mbalimbali ikiwemo haki ya kurudi nyumbani katika ardhi yao ya asili, ni miongoni mwa masuala muhimu katika mzozo unaoendelea kati ya Israeli na Palestina.
Hii ni kwa sababu wakimbizi wote wanafurahia haki ya kutambuliwa taifa lao kimataifa, kwa kurejea katika ardhi yao ya asili ambayo wao walilazimishwa kuihama na kukimbilia nje. Haki hii imekubalika waziwazi kupitia mikataba ya amani ya hivi karibuni katika nchi mbalimbali kama vile Cambodia, Rwanda, Croatia, Bosnia-Herzegovina, Guatemala, Ireland ya Kaskazini, Kosovo, Sierra Leone, Burundi, na Sudan.
Umoja wa Mataifa unatilia mkazo haki hii ya Wapalestina, kupitia Azimio lake namba 194 la mwaka 1948, lakini Israeli kwa kukwepa mkono wa sheria haikukubali kurudi kwa Wapalestina katika ardhi yao ya asili, wakati Mayahudi kutoka mahali popote duniani walipo wanaweza kurudi na kuishi nchini Israeli. Nakba ni maafa makubwa zaidi kuliko uhalifu wa aina yake wa mwaka 1948, ni janga la kihistoria ambalo bado wapalestina wanalichukulia kuwa ni ukweli na uhalisia, si tu kukumbuka tukio hilo ili kuadhimisha kilichotokea miaka 69 iliyopita, bali ni maafa yanayoendelea kuiharibu Palestina na Wapalestina wenyewe hadi leo.
Hivyo basi, siku ya Mei 15 kila mwaka,huwa si tu ya maadhimisho ya miaka 69 au zaidi ya maafa ya Nakba, bali ni mwaka mmoja zaidi wa kudumu kwa ukatili wake. Historia ya maafa ya Nakba haikuwa ni historia tu ya siku na miaka iliyopita, bali ni historia ya sasa tunayoishi nayo.
Nakba imesababisha mamilioni ya wakimbizi wa kipalestina hadi leo kusambaa duniani kote, huku wengi wao wakiwa ni wakimbizi kwa zaidi ya mara mbili au tatu, kutokana na uvamizi wa makazi yao na ardhi yao unaoendelea nchini Palestina. Uvamizi huu wa kidhalimu na uhalifu huu, unaendelea kufanywa na Israeli kinyume na sheria, ukiwemo upanuzi wa mara kwa mara wa makazi haramu ya walowezi,kupora ardhi ya Wapalestina na kuharibu mali na maisha yao.
Hivyo basi,Wapalestina popote duniani, jumuiya ya kimataifa na wale wote wapenda haki na amani duniani, huadhimisha siku hii ya Mei 15, ikiwa sio tu siku ya maombolezo na maadhimisho ya yale yaliyotokea mwaka 1948, bali pia ni siku ya kuungana na wananchi wa Palestina katika kudai uhuru wao, haki zao na kumaliza uvamizi wa kimabavu na kidhalimu katika ardhi yao ya Palestina.