MBUNGE wa Kinondoni, Maulid Mtulia (Chadema), ameliambia Bunge kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul 'Diamond Platinumz', anadaiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) zaidi ya Sh. milioni 400.
Mbunge huyo aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wasanii wengi maarufu na wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kutokana na mauzo ya kazi zao.
Alidai Diamond Platinumz amemwambia kwa sasa anadaiwa kodi ya zaidi ya Sh. milioni 400.
Kutokana na msanii huyo na wenzake kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kazi zao za sanaa, Mtulia aliiomba serikali kuhakikisha inaimarisha mapambano dhidi ya wizi wa kazi zao badala ya kutilia mkazo kwenye ukusanyaji wa kodi pekee.
Alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana kuzungumzia kauli ya Mbunge huyo, Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema suala hilo liko kwenye uchunguzi.
"Hilo liko kwenye hatua ambayo hatuwezi kulizungumzia kwenye vyombo vya habari. Liko katika 'investigation' (uchunguzi)," alisema.