Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeeleza kuwa nafasi za Wabunge wa Viti Maalum wanaoteuliwa zipo kwa mujibu wa Sheria na zimeainishwa katika Ibara ya 78 (1) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Akitoa ufafanuzi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani amesema kuwa Ibara ya 78 (1) na (4) ya Katiba inaeleza utaratibu mzima wa kuwapata Wabunge wanawake wa Viti maalum.
Amesema kila Chama cha Siasa kinachoshiriki katika Uchaguzi Mkuu na kupata angalau asilimia 5 ya Kura zote halali za wabunge kitapata Wabunge wa Viti Maalum kulingana na Kura ambazo chama husika kimepata.
Amefafanua kuwa Chama kinachopata asilimia 5 ya Kura zote halali za Wabunge katika Uchaguzi Mkuu kinatakiwa kuwasilisha orodha ya wanachama wanaopendekezwa kuwa wagombea wa Viti Maalum ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha, ameeleza kuwa endapo inatokea nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na sababu mbalimbali, Spika wa Bunge humtaarifu Mwenyekiti wa Tume juu ya uwepo wa nafasi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Amesema kuwa Mwenyekiti wa Tume hukiandikia barua chama husika kukitaarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi ya viti maalum ili kiweze kuwasilisha pendekezo la jina katika orodha kiliyowasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwaka 2015, ikiambatanishwa na Fomu namba 8 D ya kuomba jina lililopendekezwa liteuliwe na Tume katika nafasi ya Ubunge kulingana na sifa zilizoainishwa kwa mujibu wa Sheria.