Vanessa Mdee ameshindwa kuyavumilia yanayomtoka kinywani mmoja kati ya vigogo anaowaheshimu kwenye sanaa ya muziki nchini, hali iliyomsukuma kuanika ya moyoni.
Vee Money ambaye anafanya vizuri na wimbo wa ‘Duasi’ alioshirikishwa na Legendary Beatz ametumia mtandao wa Twitter kuyatoa ya moyoni dhidi ya kigogo huyo, ingawa hakuweka wazi jina lake.
“Inasikitisha kwamba mtu ninayemheshimu na kumtambua kwenye hii sanaa kila kukicha jina langu mdomoni mwake kwa kashfa zisizoeleweka,” inasomeka tweet ya kwanza ya Vee Money.
Hata hivyo, mwimbaji huyo ameamua kuweka heshima yake mbele na kujiepusha na majibishano kwani kufanya hivyo anaamini kutakuwa utovu wa nidhamu.
Inasikitisha kwamba mtu ninayemheshimu na kumtambua kwenye hii saana kila kukicha jina langu mdomoni mwake kwa kashfa zisizoeleweka .— VeeMoney #CashMadame (@VanessaMdee) May 3, 2017
Siwezi kujibishana nawewe itakuwa utovu wa nidham baba.— VeeMoney #CashMadame (@VanessaMdee) May 3, 2017
Mwaka huu umeendelea kuwa mwaka wa mafanikio ya kupanda zaidi katika ngazi za kimataifa kwa Vee Money, ingawa amekuwa akikumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kutajwa kwenye orodha ya wasanii waliotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya.
Msanii huyo ameendelea kukubalika ndani na nje ya nchi ambapo amekuwa akipewa mashavu kadhaa kung’arisha nyimbo za wasanii wa nchi za Afrika Kusini na Afrika Magharibi.