Mkazi wa kijiji cha Ijenga, Mbalizi mkoani Mbeya Sikitu Mwawala (25) ameuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi na kasha mwili wake kuchomwa moto kutokana na imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiria Kidavashari, akizungumza na Nipashe Digita leo amesema tukio hilo limetokea Mei Mosi mwaka huu saa 10:30 asubuhi katika kijiji cha Mjele.
Amesema chanzo cha mauaji hayo ni kipigo kilichotokana na kulipiza kisasi kufuatia marehemu na wenzake kutuhumiwa kuhusika katika tukio la mauaji ya mwanamke aitwaye Zaituni Saisoni (20) mkazi wa kijiji cha Katusi kilichotokea Aprili 25 mwaka huu.
Mwanamke huyo baada ya kuuawa, watuhumiwa walichukua baadhi ya viungo vyake ikiwemo matiti, masikio, macho na ngozi ya paji la uso kwa imani za ushirikina.
Kamanda Kidavashari ametoa onyo kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wajenge tabia ya kuwafikisha watuhumiwa wanaowakamata katika vyombo vya sheria.