Wakati kukiwepo na mfumko wa bei ya chakula cha nafaka ya mahindi iliyofikia gharama ya gunia lenye ujazo wa kilo 100 la mahindi kuuzwa kwa shilingi 150,000/= katika soko la Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara,baadhi ya wananchi wa halmashauri ya mji huo wamelalamikia kupanda kwa bei ya sukari kiholela hadi kuuzwa kwa bei ya shilingi 3,000/= kwa kilo moja badala ya bei elekezi ya shilingi 2,200.
Uchunguzi wa ITV uliofanyika kwenye maduka mbalimbali ya biadhaa mjini Babati umebaini kuwepo kwa mfumko wa bei ya sukari inayouzwa kati ya shilingi 2800/- hadi kufikia bei ya shilingi 3.000/= kwa kilo moja huku baadhi ya wauzaji wa maduka ya rejareja wakilalamikia ununuzi wa sukari umekuwa wa kusuasua.
Hata hivyo Afisa biashara wa Halmashauri ya mji wa Babati Bw Anthony Mkakate amethibitisha kupanda kwa bei hiyo ya sukari na kudai kuwa kutokana na kuwepo kwa ukiukwaji wa bei elekezi na kufungwa kwa kiwanda cha TPC kwa ajili ya matengenezo ya msimu ni miongoni mwa sababu huku,baadhi ya wafanyabiashara wasambazaji wakikiri bei kubwa wanayokabiliana nayo.
Mfuko huo wa bidhaa ya sukari unaosababisha kikombe cha chai ya rangi kuuzwa kwa bei ya kuanzia shilingi 300 hadi 500 umelalamikiwa na baadhi ya wananchi wenye kipato kidogo kushindwa kunywa chai,huku pia kukiwepo kwa mfumko wa bei ya nafaka ya mahindi.