Baadhi ya wananchi Wa Kara ya Olasiti kama wanavyoonekana pichani.Picha na Vero Ignatus blog.
Na .Vero Ignatus,Arusha.
WAKAZI wa Olasiti jijini Arusha wamesusia maji yanayotolewa na Idara ya maji na kudai kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya aina yoyote.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanywa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo wananchi hao walisema maji yaliyosambazwa na Idara ya maji yana chumvi kiasi cha kuharibu hata mimea wanapojaribu kumwagilia.
Mmoja wa wakazi hao Meck Mollel alisema wanahofia baada ya miaka ijayo kutokuwa na nguvu za kiume kutokana na kuendelea kutumia maji hayo ambayo yanaladha ya magadi.
"Kweli haya maji yanatupa hofu baadaye tutajikuta wanawake wote kwa mpango huu hatuyahitaji haya maji tuleteeni maji yaliyorafiki kwa binadamu" alisema Mollel.
Naye mkazi mwingine alisema maji hayo akiwapa vifaranga wanapata matege kutokana na hali ya chunvi iliyozidi ambapo pia alisema akimwagilia mimea inakuwa ya njano.
Hata hivyo mkuu wa mkoa aliwataka wananchi hao kufahamu kuwa serikali haiwezi kuruhusu maji yasiyo faa kwa matumizi ya binadamu hivyo maji hayo yalipimwa na kuonekana yanafaa ndio maana yakaruhusiwa.
"Serikali yoyote duniani haiwezi kuruhusu kitu chenye madhara kwa wananchi wake hivyo tutaleta tena wataalamu kuyapima tena na majibu yatakayopatikana tutajua cha kufanya" alisema Gambo.
Naye Mkurugenzi wa maji jiji la Arusha Ruth Koya alisema kiwango cha maji salama hakipimwi kwa macho bali kinapimwa maabara hivyo wataalam wamepima na wakaona yanafaa kwa matumizi.
Koya alisema maji wanayolilia wananchi hao yanafloride lakini hayo yaliyopo pamoja na kuwa na chumvi hayana madhara kwa matumizi Kama wanavyolalamika wao..