Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa tamko kuhusu Siku ya Malaria Duniani kwa waandishi wa Habari Mjini Dodoma na kusisitiza kuwa vipimo vya Malaria na Dawa za Mseto ni bure kwa vituo vyote vya Afya vya Umma nchini.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuzindua Kitabu cha Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria katika kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi kutoka kamouni ya Gullin Pharma mara baada ya kuzindua Kitabu cha Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria katika kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani. Picha zote na Raymond Mushumbusi Dodoma MAELEZO.
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO Dodoma.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali haitosita kuwachukulia hatua mtumishi yoyote katika vituo vya Afya vya Umma nchini watakaobanika kutoza fedha katika kutoa huduma ya vipimo vya malaria na kuuza dawa za Mseto kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo.
Ameyasema hayo Mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari kutoa tamko la Siku ya Malaria Duniani na kusisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kupata huduma ya kupima malaria pamoja na dawa za kutibu malaria bure katika vituo vya Afya vya Umma.
“Huduma ya kupima Malaria na dawa za Mseto zinatakiwa kutolewa bure katika vituo vyote vya Umma vya Huduma za Afya nchini na hatutosita kuwachukulia hatua watakaokiuka kutekeleza agizo hili.Alisistiza Mhe. Ummy.
Aidha amwewaagiza Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza agizo hilo na kulisimamia kwa karibu ili kuondoa usufumbu kwa wananchi wanapotaka kupatiwa huduma hiyo.
Mhe Ummy Mwalimu amewashukuru wadau wote waliochangia kwa hali na mali katika mafanikio yaliyofikiwa ya mapambano ya dhidi ya Malaria nchini.
Siku ya Malaria Duniani uadhimishwa kila Aprili 25 ya kila mwaka na kwa mwaka huu kauli mbiu ni “ Shiriki kutokomeza Malaria kabisa kwa Manufaa ya Jamii”.