Baada ya kupigwa marufuku kwa pombe zilizokuwa zinafungwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu viroba, baadhi ya vijana Manispaa ya Shinyanga wameanza kutumia ugoro kwa kasi wakidai ni mbadala wa pombe hiyo.
Kutokana na ongezeko la watumiaji, bei ya ugoro imepanda kutoka Sh200 hadi Sh500 kwa kijiko.
“Kijiko kimoja cha ugoro kinatosha kupata stimu na inapatikana kwa Sh500 kuliko mtu kutumia zaidi ya Sh2,000 kununua chupa moja ya bia,” alisema Hogo Yola, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga anayetumia ugoro kama kilevi.
Mtumiaji mwingine wa ugoro, Ezekiel Laizer, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga alisema tangu alivyoanza kutumia kilevi hicho, amepata nafuu ya kukaa muda mrefu akiwa amelewa kama ilivyokuwa wakati akitumia viroba.
Daktari wa Afya ya Kinywa na Meno Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dk Daniel Maguja alisema kitaalamu ugoro una sifa ya kuwa na uwezo wa kugandamiza sehemu ya ubongo, hivyo kumfanya mtumiaji kupata msisimko na papo hapo kutosikia kiu sawa na wanaovuta sigara.