Rais John Magufuli amesema kati ya madaktari 500 walioonyesha nia ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya watachaguliwa 258 na kuajiriwa na serikali ya Tanzania mara moja kuanzia sasa.
Taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ilieleza kuwa hatua hiyo imefuatia baada ya kutetereka kwa makubalino ya serikali ya Tanzania na Kenya baada ya Mahakama nchini Kenya kutoondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za madaktari wa Tanzania nchini humo.
“Rais Magufuli ameamua kuwa, madaktari hao 258 ambao walikuwa tayari kwenda kufanya kazi nchini Kenya waajiriwe na serikalini mara moja. Kufuatia uamuzi huu, majina ya madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya wizara www.ehealth.go.tz pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo,” amesema Ummy.