Moja ya mitambo ya maji katika eneo la Ruvu Juu kama inavyoonekana, mitambo hii ni mipya na kwa sasa ndiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa maji toka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku.
Hii ni sehemu ya mtambo wa kusafirishia mai mara baada ya kusafishwa, hapa ndipo maji hukusanywa na kusafirishwa moja kwa moja kuelekea kwa wananchi.
Hii ni sehemu ya mtambo unaotumika kuwashia mitambo ya kusukuma maji katika eneo la Ruvu Juu.
Laini ya Umeme unaotoka Chalinze (Sub-Station) na kufika eneo la Mtambo wa Ruvu Juu lililopo Mlandizi Mkoani Pwani.
Laini ya Umeme unaoingia kutoka Chalinze (Sub-Station) na kufika eneo la Mtambo wa Ruvu Juu lililopo Mlandizi Mkoani Pwani ambapo uunganishaji wake sasa umeshakamilika na umeme umewashwa.
Moja ya Transfoma mpya zilizopo katika eneo la Mtambo wa Ruvu Juu ambalo linatumika kutoa umeme unaotumika kwenye mitambo katika eneo hilo.
(PICHA/HABARI NA MWANDISHI WETU)
Baada ya kazi ya kuunganisha umeme wa kutosha kukamilika 15 Aprili, 2017 kazi ya kuwasha pampu kubwa mpya za majighafi na majisafi katika Mtambo wa Ruvu Juu sasa imekamilika rasmi ambapo mtambo huo sasa umeanza kuzalisha lita milioni 196 kwa siku. Taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar Es salaam (DAWASA) inaeleza.
Ili kufikia uwezo huo wa uzalishaji kutoka lita milioni 82 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali, kazi mbalimbali zilifanyika ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji na ufungaji wa pampu mpya, maeneo mapya ya kusafisha maji, mitambo ya kuchuja maji, maeneo ya kuchuja tope na tenki kubwa la kuhifadhia maji safi.
Katika kuhakikisha kuwa maji hayo yanawafikia wananachi, kituo kipya cha kusukuma maji safi na salama kilijengwa sambamba na mabomba makuu ya kusafirishia maji hayo yenye jumla ya urefu wa kilomita 70 kutoka Mlandizi hadi Dar es salaam.
Aidha, tenki jipya lenye uwezo wakuhifadhi lita milioni 10 limejengwa eneo la Kibamba lenye mwinuko; na kutoka hapo maji hushuka kwa nguvu ya mtiririko hadi katika matenki ya Kimara.
Kazi iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kuongeza nguvu ya umeme ili kuwezesha pampu hizo mpya kufanya kazi. Hivi sasa kazi hiyo imekamilika, ukaguzi umefanyika na pampu moja baada ya nyingine zimewashwa ili kuhakiksha mfumo mzima sasa unafanya kazi.
Hadi kufika jana jioni (17 Aprili) maji yalikuwa yanaingia katika matenki yote kwa kupitia mabomba mapya bila matatizo.
Mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu sasa unapokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo kituo kidogo cha umeme cha Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo inawezesha pampu zote mpya na za kisasa zilizofungwa kuwashwa kwa wakati mmoja.
Mikataba ya jumla ya dola za Marekani milioni 99 ya upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara, ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 10, ofisi kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa huduma na nyumba za watumishi wa mtambo ilisainiwa mwaka 2014. Fedha hizo zilikuwa ni mkopo wa masharti nafuu toka Benki ya Exim ya India.
Kazi inayopewa msukumo mkubwa kwa sasa ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yaliyoongezeka ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na jitihada na uwekezaji uliofanywa na Serikali yao.
Maeneo yanayonufaika ni pamoja na miji ya Kibaha, Mlandizi na baadhi ya Vitongoji vyake katika mkoa wa Pwani pamoja na maeneo yote yaliyopo jirani na barabara ya Morogoro yaani Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo, Malamba mawili, Msigani, Msakuzi, Makabe, Kibangu, External, Makuburi, Tabata, Segerea, Buguruni pamoja na Vingunguti.