Wakati wa kutafuta kazi, mara nyingi kuna kuchoka na ukifanikiwa kupata kazi unaweza kujikuta unachukua kazi bila kufikiri vitu vingi sana. Usipofikiri vizuri kazi hiyo inaweza kukugharimu fedha nyingi na kupoteza muda wako kwa kiasi kikubwa. Kama unafanya kazi za mjini na unapanga kusafiri kutoka nyumbani kwenda kazini inakubidi ujue umbali unaoishi, tafuta usafiri wa uhakika kwa kuangalia vigezo vifuatavyo.
1. Je utasafiri vipi kutoka nyumbani kwenda kazini?
Je utaendesha gari kutoka nyumbani kwenda kazini? utapanda daladala, je kuna usumbufu gani wa mimi kutumia gari yangu ama kutumia daladala? Je itanigharimu kiasi gani kwa kutumia gari yangu kila siku kwenda kazini? Na nikitumia daladala itanigharimu kiasi gani? je nitatumia muda kiasi gani barabarani? Hivyo kabla ya kukubali kuchukua kazi jaribu kuwaza namna ya kufika kazini kila siku na gharama zake kifedha na muda.
2. Gharama za usafiri zinaathiri vipi kipato changu?
Wakati wa kuangalia gharama fikiria pia hizo gharama zinaathiri vipi kipato chako au mshahara wako. Watu wengi wanafanya makosa baada ya kujenga nyumba hukimbilia kuhamia huko bila kuangalia gharama zinazoambatana na kuishi mbali. Ingawa tunaangalia adha ya kodi ya nyumba, hatufikirii usafiri na muda utakaotumia barabarani na namna utakavyoathirika kimapato na maisha ya kifamilia.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
3. Muda wako wa kazi ukoje?
Hakikisha unajua muda wako wa kazi ukoje, unapaswa kuingia kazini saa ngapi na unatakiwa kutoka saa ngapi. Je familia yako itaathirika vipi na muda wa wewe kuondoka nyumbani na kurudi kila siku? Je utaweza kuiona familia yako kila siku kabla hawajaenda kulala?
4. Kuna fursa gani mpya kwenye kazi hiyo mpya?
Unatakiwa kujua fursa inayoambatana na kazi hiyo, ukiondoa mshahara mzuri kuna nini kipya? Je taaluma yako itakua? utajifunza nini? Je unatakiwa ujue kazi hiyo ni kwa muda gani? Ni kwa muda mfupi au mrefu na wewe una mipango gani?
5. Je unaweza kufanya kazi karibu na nyumbani?
Kama kazi unayopata haitakufanya kuwa mbali na nyumbani au kusafiri masaa mengi, ni vizuri kuifikiria kazi hiyo kuliko kwenda mbali.
6. Fikiria kuhama makazi?
Kama kusafiri muda mrefu kutoka kazini kwenda nyumbani kumeathiri mapato yako, maisha yako na familia yako ni wakati wa wewe kufikiria kuhamia karibu na eneo ambalo litakuwezesha kufika kazini na kupunguza gharama fulani fulani. Itakusaidia kuanza maisha mapya na kukutana na watu wapya.
Wakati unafikiri kusafiri, usisahau maswali ya msingi yatakayokuwezesha kuyatazama mambo kwa undani wake bila kupoteza fedha na muda wako. Kuna maisha baada ya kazi unahitaji ugunduzi tu!