Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal, katika Mkutano wa mwaka wa Uzazi wa Mpango, Oktoba mwaka huu. Katika Mkutano huo Tanzania ilionekana bado ina matumizi ya chini ya dawa za uzazi wa mpango. Picha na Maktaba.
Pamoja na kuwa ni njia nzuri ya kuzuia ujauzito, vidonge vya Uzazi wa Mpango vinatajwa kusababisha ugonjwa wa macho ujulikanao kamaGlaucoma, unaoelezwa kuwa ni chanzo kikuu cha upofu.
Ugonjwa huu unaelezwa kuwa sababu kubwa ya kusababisha upofu kwa wanawake wanaotumia vidonge hivi kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa kwenye Utafiti wa Afya na Lishe uliofanywa na Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa cha Marekani(CDCP).
Utafiti huo unasema kuwa, seli zilizoko katika neva za macho zina homoni za estrogen ambazo hufanya kazi ya kulinda macho, vidonge hivyo huingilia mchakato huo wa ulinzi kwa kupunguza kiwango cha homoni hizo.
Unasema kuwa wanawake wanaofunga hedhi mapema au wanaotumia vidonge ambavyo huzuia kuzalishwa kwa vichocheo vya estrogen, na dawa za saratani ya matiti, huweza kupata upofu.
Wanawake zaidi ya 3,400 wenye umri wa zaidi ya miaka 40 walifuatiliwa kwa zaidi ya miaka mitano ikiwa ni sehemu ya utafiti huo.
Profesa Shan Lin wa Chuo Kikuu cha Carlifonia, San Francisco anasema wanawake wanaotumia vidonge hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu, wanatakiwa kupima maradhi ya macho aina ya Glaucoma na afya zao zifuatiliwe kwa uangalifu na wataalamu wa macho.
Utafiti huo umebaini kuwa wanawake waliotumia vidonge hivyo kwa miaka zaidi ya mitatu walikuwa na hatari kwa asilimia tano ya kupata upofu usababishwao na glaucoma ukilinganisha na wasiotumia vidonge hivyo.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Louis Pasquale wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Havard anasema vichocheo vya Estrogen vina umuhimu katika seli za retina ambazo zinajulikana kwa kupokea homoni hizo.
“Kuwepo kwa homoni za estrogen kunazisaidia seli hizo kuwa hai kwa hiyo wanawake wanapotumia vidonge vya uzazi, homoni hizo huharibiwa na kurahisisha uharibifu wa macho,” anasema Dk Pasquale.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk Cyriel Masawe wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (MNH) anasema ni hatari kwa wasichana wadogo ambao hawajaolewa kutumia dawa hizo ovyo.
“Kwa mfano mikoa ya Lindi na Mtwara, tumegundua wasichana wadogo ambao hawajaolewa wanatumia zaidi sindano za uzazi wa mpango na vidonge,” anasema
Dk Masawe anasema si vyema watu kuzitumia dawa za Uzazi wa Mpango kwa mazoea na endapo wataona ni vyema kufanya hivyo, washauriane na wataalamu wa afya.
Anasema kuwa elimu inahitajika kwa kina kuhusu matumizi ya dawa hizo kwani wapo baadhi ya watu wanaozitumia bila mpangilio wala utaratibu maalum.
“Hizi dawa zinasaidia lakini zisipotumiwa kwa uangalifu, huenda zikasababisha madhara,” anasema Dk Masawe.
Kwa upande wa utafiti huo uliojikita kuangalia madhara ya vidonge hivyo kwa wanawake, watu wanaovitumia wanatakiwa kuwa makini na uhusiano uliopo kati ya afya ya uzazi na maradhi ya macho hasa kama mtumiaji amefunga hedhi mapema.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa katika mkutano wa kila mwaka wa Chuo Kikuu cha Mfumo wa Macho Marekani (USP), yanasema wanawake zaidi ya 3,046 walifanyiwa uchunguzi kuhusu afya ya uzazi na maradhi ya macho.
Pamoja na sababu nyingine za maradhi ya macho, wanasayansi waliofanya utafiti huo wanasema kutumia vidonge vya uzazi kwa muda mrefu, ndicho chanzo kikuu cha upofu na kutaja sababu nyingine kuwa ni historia ya familia, shinikizo la ya macho na kisukari.
Watalaamu wa afya nchini wanasema bado madhara ya dawa hizo yanatofautiana kulingana na aina ya dawa anayotumia mhusika.
Madhara mengine ya dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu, kichwa kuuma, matiti kuuma, kuongezeka uzito na kupata hedhi bila mpangilio.
Dk Joseph Matiku wa Kituo cha Afya, Mugumu, Serengeti anasema, hatari zaidi ni kwa binti wanaotumia dawa hizo kwa muda mrefu kabla hawajaanza maisha ya ndoa.
“Wapo wanawake ambao wanapata uvimbe kwenye kizazi kutokana na matumizi ya muda mrefu ya dawa hizi. Ingawa hakuna utafiti uliofanyika kuthibitisha hili, lakini wanawake wengi wanaotumia dawa hizi hapa nchini wanapata uvimbe maarufu wa Fibroids” anasema.
Hata hivyo, Oktoba mwaka huu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi anasema Wizara ya Afya ipo kwenye harakati za kutafuta fedha ili kuhakikisha asilimia 60 ya wanawake wanaostahili kupanga uzazi wanapata dawa husika.
Mwaka jana wakati wa Mkutano wa Uzazi wa Mpango uliofanyika London Uingereza, Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuwa hadi kufikia mwaka 2015 Tanzania itafikisha asilimia 60 katika huduma za uzazi wa mpango.
Vilevile katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Uzazi wa Mpango uliofanyika Oktoba mwaka huu, Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal alisema juhudi za ziada zinahitajika kuhakikisha kiwango cha watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango, kinaongezeka ili kutimiza lengo la kimataifa ya kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hiyo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa, kiwango cha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango kwa nchi zilizoendelea ni asilimia 72, huku Tanzania iliyo kwenye kundi ya nchi zinazoendelea ikiwa ni asilimia 27 tu.
Dawa za uzazi wa mpango hufanyaje kazi?
Vidonge vya uzazi wa mpango hufanya kazi ya kuweka uwiano katika kiwango cha vichocheo.
Katika hili, kazi kubwa ni kuzuia homoni za estrogen kuongezeka na kufikia kiwango cha kati au cha juu.
Bila homoni ya estrogen, tezi ya pituitari haiwezi kuifanya mirija ya uzazi kuruhusu mayai yaliyochavushwa kwenda kukutana na mbegu za kiume kwa ajili ya utungishwaji wa mimba.
MWANANCHI