Maisha yanavyokwenda unahitaji kuwa mtu mwangalifu na nani yuko karibu yako. Unahitaji mshauri wa mambo yako ya karibu, kama biashara, Maisha kwa ujumla, ndoa, taaluma na hata Kiroho. Kuwa na mshauri ni dhana ambayo watanzania wengi hatujaizoea na hufikiri tunaweza kufanya kila kitu, lakini mambo yako yanakuwa bora zaidi unapokuwa na mshauri mwenye uzoefu mkubwa kuliko wewe na aliyekutangulia kwa namna fulani.
Fikiria kuhusu wewe mwenyewe, Je unahitaji mshauri?
Watu wengi huwa tunajitahidi kujilinda ili tusijulikane makosa yetu au udhaifu tulionao kwenye biashara, taaluma, ndoa na hata maisha ya kawaida. Ukweli ni kwamba bado hujafika kiwango unachotakiwa kufika, unahitaji ushauri hasa kwa kile unachofanya. Ikiwa wewe ni kiongozi tafuta kiongozi bora kuliko wewe apate kukusaidia mambo kadha wa kadha.
Mshauri wako anahitajika kuwa mtu mwenye uadilifu mkubwa, aliyefanikiwa, mwenye hekima na upeo mkubwa kimaisha na hata kifikra. Si kila unayemwona mbele yako anaweza kukushauri hata kama ni mkubwa kuliko wewe, hapa sizungumzii ndugu, nazungumzia mtu ambaye yuko tayari kukwambia ukweli na kukusaidia.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Tumekuwa na hulka ya kuwaheshimu watu fulani labda kwa sababu ya madaraka yao, fedha na nguvu walizonazo lakini inapokuja suala la maisha yako binafsi kazini, nyumbani , kwenye uongozi na biashara unahitaji mtu mwenye akili timamu.
Mtu ambaye ndoa yake inayumba hawezi kukusaidia ndoa yako kiushauri, hiyo sahau. Mtu ambaye biashara hajui au hajawahi kufanya biashara usitegemee kuwa anaushauri wa kukuza biashara yako. Huweza kukaa chini ya mkwaju halafu unategemea kuvuna maembe. “Fikiri na chukua hatua”
Fanya Uchunguzi kuhusu mtu anayetakiwa kukushauri.
Hapa ndipo unaweza kuyakoroga mambo, watu wengi tunaangalia uwezo wa kifedha, madaraka na umaarufu, sahau hayo yote angalia uadilifu, ndoa yake ina msimamo au yeye mwenyewe ana msimamo au ni kiruka njia? Kama ni mfanyabiashara fanya uchunguzi wa biashara zake, anafanya biashara na nani, utu wake ukoje na hali yake ya kiroho imekaaje? Je ni muumini mwadilifu au haeleweki? kama haeleweki hata maadili yake hayaeleweki.
Ukisharidhika na uchunguzi wako, chukua hatua ya kumwomba kuwa mshauri wako kwenye jambo ambalo unaona anafaa. Akikubali endelea naye akikataa endelea kutafuta mtu mwingine. Wakati wa kuishi kufuata mkumbo umekwisha, ni sawasawa na kuishi maisha ya wengine na maisha yako hujawahi kuishi.
Nitafurahi kusikia kutoka kwako ndugu msomaji wetu. Siku jema!