Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiingia bungeni mjini Dodoma jana kuhudhuria semina ya kuchangia taarifa ya Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge kuhusu Kanuni. Picha na Silvan Kiwale
Hofu imetanda kuhusu uwezekano wa kuvunjika kwa Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na hatua ya CCM kutumia wingi wao kutaka kupitisha utaratibu wa kupiga kura za wazi.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wameshauri njia pekee ya kunusuru mchakato huo ni kwa CCM kukubali kukaa meza ya mazungumzo.
Wakati wajumbe hao wakitoa angalizo hilo, taarifa zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema CCM, wameitisha kikao cha dharura cha wajumbe wake wote leo saa 8:00 mchana kwa agenda ambayo bado ni siri.
Habari hizo zinadai kuwa wajumbe ambao ni Wabunge na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wametumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) wakitakiwa kuhudhuria kikao hicho bila kukosa.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Mambo muhimu yatajadiliwa, Mwenyekiti wa Cocas (umoja wa wabunge) anasisitiza mhudhurie bila kukosa, mahudhurio yatazingatiwa,” unasomeka ujumbe huo ambao gazeti hili limeuona.Baadhi ya wabunge wa CCM hususan wanaotoka Kanda ya Ziwa wanaounga mkono kura ya siri, walidai kuwa kikao hicho huenda kina nia ya kuwatisha ili walegeze msimamo wao.
“CCM wanaogopa kura za siri kwa sababu moja tu, wakiiruhusu watakuwa hawana control (udhibiti) wa wajumbe kutoka Zanzibar ambao wengi wanataka Serikali tatu,” alidokeza mbunge mmoja ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe.
Mbunge huyo alisema kwa tathmini yake, kama utaratibu wa kura za siri utapita, karibu asilimia 80 ya wajumbe wote kutoka Zanzibar, watapiga kura ya kupitisha rasimu ya muundo wa Serikali tatu.
“Kwa hiyo CCM haitaki kabisa utaratibu wa kura za siri, wanataka kura za wazi ama kura ya dhahiri ili waweze kuwa na udhibiti wa wajumbe ili tusitoke nje ya msimamo wao,” alidai mbunge huyo.
Hata hivyo, wakati CCM ikishikilia msimamo wa kura za wazi katika kupitisha rasimu hiyo, wabunge wake wengi wa Tanzania Bara na wale wa Zanzibar wanataka upigaji wa kura za siri.
Akizungumza na gazeti hili jana, James Mbatia alitahadharisha kuwa msimamo wa CCM kulazimisha kura za wazi, siyo kuwatendea haki Watanzania na huenda ikawa chanzo cha machafuko na kukwama kupatikana Katiba Mpya.
“Kulazimisha matakwa ya CCM badala ya wananchi itakuwa ni chanzo cha machafuko na Watanzania hatuko tayari kwa machafuko wala kuona damu ya Mtanzania inamwagika,” alisema Mbatia
Mbatia aliongeza kusema; ni vizuri hiyo Rasimu ya Katiba tuiboreshe, tupunguze mengine na CCM kama wana hoja wazilete bungeni na ziwe hoja zenye mashiko siyo vitisho, hatutavuka hapa.”
Mbatia aliwataka baadhi ya viongozi wa CCM kutokujifanya wanamfahamu sana Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuliko anavyomfahamu Joseph Butiku na Joseph Warioba walioshiriki kukusanya maoni ya Watanzania kwa ajili ya Katiba Mpya.
“Nyerere hakuwa na mawazo mgando, alikuwa na fikra pevu zilizokuwa zinakwenda na wakati na ndiyo maana alikubali mapendekezo ya Watanzania asilimia 20 waliotaka mfumo wa vyama vingi,” alisema.
Alisema kama kweli viongozi wa CCM wana dhamira ya kweli na muundo wa Muungano, basi wafute kwanza mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ili sasa wazungumze.
“Mabadiliko ya 10 ya Zanzibar yalitamka kuwa Zanzibar ni nchi na ina mipaka yake na mwenye mamlaka ya kuigawa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar… hilo tu tayari walikuwa wamevunja Katiba ya Muungano.
Mbatia alisema ibara ya 2(A), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, imeweka bayana kuwa pale Rais anapotaka kuigawa Zanzibar, atashirikiana na Rais wa Tanzania Zanzibar.
“Kwa katiba hiyo, Rais wa Zanzibar amepora ardhi ya JK (Rais Jakaya Kikwete) kwa hiyo walishavunja Muungano kisheria… kwa maneno mengine mabadiliko hayo ni uhaini dhidi ya Katiba ya Muungano.”
Mbatia alisema katiba siku zote ni tendo la maridhiano na kuitaka CCM kuingia katika maridhiano, kama kweli ina nia thabiti ya kuwapatia Watanzania katiba badala ya kutumia wingi wao kuififisha.
Mwenyekiti huyo alisema anawashangaa CCM kwamba wao ndiyo walioanzisha mchakato wa katiba na kuunda tume, mchakato ukaendeshwa na Serikali ya CCM halafu wanayakataa mapendekezo yake.
Mbatia alisema tume tano zilizoundwa kwa ajili ya suala moja tu la muundo wa Muungano, zilikuja na mapendekezo ya Serikali tatu na kushangaa CCM sasa kuhoji uadilifu wa Tume ya Jaji Warioba.
Tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba, bunge hilo limetumia takriban siku 16 sasa katika kutunga rasimu za kanuni na kubwa linalobishaniwa ni utaratibu wa upigaji wa kura.
Mapendekezo ya awali ya Kanuni za Uendeshaji wa bunge hilo, zilipendekeza upigaji kura uwe wa siri na hata wajumbe walipochangia na CCM kung’ang’ania kura za wazi, bado kamati ilikuja na pendekezo la kura za siri.
Hata hivyo wajumbe wengi wanaotoka CCM walipinga kwa nguvu zote kura za siri wakitaka za wazi na suala hilo kurudishwa kwenye kamati, lakini hadi juzi kamati ilishindwa kuafikiana.
Kutokana na suala la upigaji kura kuonekana ni tata, kamati iliyoundwa kupitia kauni hizo, juzi iliamua kurudisha suala hilo kwa Bunge la Katiba ili ilifanyie uamuzi.
Oluoch ataka hati ya Muungano ipelekwe mezani
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekiah Oluoch, ameuchambua Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na kutaja kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo kutokugawiwa hati ya Muungano kuwa moja ya kasoro kubwa zinazoukabili.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Oluoch alihoji mantiki ya wajumbe wa Katiba kujadili Muungano, wakati hawana hati ya Muungano iliyosainiwa na waasisi wake; Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
“Mimi nililiona hilo mapema, nikaenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, nikamuuliza kama atagawa hati ya Muungano kwa wajumbe, lakini inaonekana hakuna mpango huo. Sasa tunajadilije Muungano wakati hatujui msingi wake,” alihoji.
Oluoch alisema nguzo ya Bunge la Katiba ni Muungano na kwamba matunda yake yataonekana kama kumewekwa mazingira mazuri ya kuujadili.
“Lakini utajadilije Muungano wakati huna nakala ya article of Union (hati ya Muungano). Mimi nilidhani ili kwenda vizuri wajumbe wapewe kwanza nakala ya hati hizo,” alisema.
Wawakilishi Zanzibar washikana mashati
Mwinyi Sadallah anaripoti kutoka Zanzibar kuwa wakati Bunge la Katiba linaanza kesho mjini Dodoma, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) wamesema kuna waraka bandia umesambazwa ukieleza Baraza hilo limeazimia kwa pamoja kutaka mamlaka kamili ya mataifa ya Zanzibar na Tanganyika.
Waraka huo umesababisha mgogoro na kutoelewana kwa wajumbe katika kamati ya uongozi chini ya Mwenyekiti wake Spika Pandu Ameir Kificho na Katibu wa kamati hiyo Yahaya Khamis Hamad, baada ya kujitokeza hadharani baadhi ya wajumbe wakisema waraka huo umeghushiwa na hawautambui.
Akizungumza na Mwananchi Spika Pandu Ameir Kificho hakukubali au kukataa kuwepo kwa waraka huo na badala yake akasema atakuwa tayari kuutolea maelezo atakapofika ofisini kwake, licha baadaye alipopigiwa simu na kupokea akasema tena kuwa atautolea majibu alasiri, jana jioni.
“Sina la kusema kwa sasa, acha nifike ofisini nitakueleza kuhusu jambo hilo...niache ndugu yangu nifike ofisni kwangu kwanza. Tafahali niko njiani hivi sasa, siko tayari kuuzungumzia waraka huo au mwingine…niache nitakwambia baadaye ,” alisema Spika Kificho ambaye ni Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alipopigiwa simu Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yahya ili atoe maelezo ya kina kuhusu waraka huo iwapo BLW Zanzibar lilitoa azimio lake na kuliwasilisha kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabailiko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba kutaka mfumo wa serikali tatu. Awali alikubali na kukana akisema inawezekana si waraka huo anaouzungumzia ila BLW limependekeza kupatikana kwa mamaka huru ya Tanganyika na Zanzibar.
“Hapana waraka wa Azimio la Baraza kutaka mfumo wa serikali tatu siutambui.Lililofanyika ni kutaka mamlaka huru za Tanganyika na Zanzibar, pia kuna mambo mengi humo, sitaki unihukumu kwa waraka ambao sioni katika simu. Ingefaa niuone kwa macho yangu kama ndiyo wenyewe au la,” alisema Yahya.
Akiuzungumzia waraka huo, Mnadhimu ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo, Salmin Awah Salmin (Magomeni), alisema waraka upo ila ni wa kughushiwa kwa sababu hakuna kikao cha kamati ya uongozi kilichowahi kukaa na kutoa azimio la pamoja juu ya aina gani ya Muungano unaotakiwa kuzingatiwa katika uundwaji wa Katiba Mpya ya Tanzania.
Salmin alisema kuwa waraka huo umeandikwa kwa niaba ya kamati ya uongozi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na una saini ya Spika wetu Kificho jambo ambalo alisema si la kweli bali ni la upotoshaji mkubwa.
Alisema kumbukumbu zinaonyesha tangu kuanza kwa mjadala wa mabadiliko ya katiba, BLW Zanzibar halijatoa msimamo wa pamoja na kuzingatiwa, badala yake kila upande wa kisiasa na kiitikadi umekuwa na maoni yake ikiwa ni pamoja na kambi ya upinzani kutaka mfumo wa Serikali ya Muungano wa mkataba na chama tawala kusimamia mfumo wa Serrikali mbili.
Mnadhimu huyo alisema baaada ya kufuatilia kwa undani aligundua kuwa kuna watu watano ndiyo waliojifungia na kuutengeneza waraka huo ukitumia jina la Kamati ya Uongozi na kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuutayarisha na kujenga hoja wanazozitaka wao kwa matakwa yao.
MWANANCHI