Quantcast
Channel: PAMOJA BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

MJUMBE BUNGE LA KATIBA AFUKUZWA

$
0
0

MJUMBE wa Bunge la Katiba, Rashid Yussuf Mshenga amefukuzwa uanachama wa Chama cha Wakulima (AFP). Kitendo hicho kimefanywa na Mwenyekiti wa chama hicho, Said Soud. Hata hivyo, Mshenga amepinga kitendo hicho na kudai ni matokeo ya wivu wa maendeleo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka bungeni Dodoma, Mshenga ambaye ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa chama hicho, alisema yeye amechaguliwa baada ya kuonekana kwamba anazo sifa na vigezo vyote.
Alisema uamuzi uliochukuliwa na Mwenyekiti wa kumfukuza ni kuonesha wivu wa yeye kutochaguliwa kuingia katika Bunge la Katiba.
“Mimi jina langu ndiyo lililopata bahati ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba, sasa sijui kosa langu lipo wapi? Huo ni wivu kwa sababu yeye hakuchaguliwa licha ya kupeleka jina lake na mkewe,” alisema.
Aidha, Mshenga alisema Mwenyekiti wa chama hicho, hana uwezo wa kumfukuza uanachama, isipokuwa Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa. Hata hivyo, kauli hiyo ya Mshenga ilipingwa vikali na Soud alipozungumza na waandishi wa habari.

 ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
 
Soud alieleza kuwa Mshenga amefukuzwa katika chama hicho baada ya kufanya kosa la kugushi saini ya Naibu Katibu Mkuu wa chama katika majina yaliyopelekwa Ikulu Zanzibar.
“Tunamfukuza Mshenga, kwa sababu ametenda kosa la kugushi saini ya Naibu Katibu Mkuu wa chama ili jina lake liingizwe katika mchakato wa majina ya chama hicho,” alisema.
Alisema Mshenga kwa wadhifa wake, anaweza kufukuzwa uanachama na Mwenyekiti; na si Mkutano Mkuu wa chama hicho.
“Cheo chake cha Mkurugenzi wa Sera na Mawasiliano anaweza kufukuzwa bila ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu...ni nafasi nne tu za viongozi ambao kufukuzwa kwake lazima kupate baraka za Mkutano Mkuu,” alisema.
Soud alikiri kuwa ni kweli alipeleka jina lake na mkewe, Farida Khamis Juma. Alisema hakuna kosa, kwa sababu mkewe anazo sifa zote, ikiwemo ni mwanachama halali, ambaye alikuwa miongoni mwa wanawake mstari wa mbele waliokiunga mkono chama hicho.
Aidha, aliilaumu Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar kwa kushindwa kufanya uchambuzi, unaotokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambaye aliagiza wenyeviti wote wa vyama vya siasa, kupewa kipaumbele katika mchakato wa Bunge la Katiba.
Alisema ameshangazwa kuona kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa AFP Tanzania nzima, lakini hakuteuliwa kuwa mwakilishi katika Bunge la Katiba.

HABARI LEO

Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>