“Baada ya kuonekana raia wamefariki kukatokea ushawishi wa kutaka baadhi ya watu wabebe dhamana ya askari ambao walionekana hawajatekeleza majukumu yao inavyotakiwa.” Nchimbi
Songea/Dodoma/Moshi. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amesema yeye pamoja na mawaziri wenzake watatu walikubali kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na askari waliokuwa wakitekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili.
Dk Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini (CCM), alisema kuna uhalifu wa hali ya juu katika mbuga za wanyama, ambao baada ya miaka 10 unaweza kumaliza wanyama kwenye mbuga hizo.
Akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Songea kwenye Viwanja vya Kiblang’oma, Kata ya Lizaboni Songea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuwasaka majangili na kuwatokomeza.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema katika operesheni hiyo, wananchi wapatao 11 na askari sita waliuawa jambo lililosababisha matatizo makubwa...
“Baada ya kuonekana raia wamefariki kukatokea ushawishi wa kutaka baadhi ya watu wabebe dhamana ya askari ambao walionekana hawajatekeleza majukumu yao inavyotakiwa.”
Alisema yeye na wenzake waliwajibika baada ya kutafakari kazi inayofanywa na askari katika nchi hii kwani wanalala usiku na kung’atwa na mbu kwa ajili ya wananchi, pia wanapambana na majambazi na hata kupoteza maisha wakati mwingine wakati wakilinda raia.
Hata hivyo, alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa heshima kubwa ya kumsaidia katika kipindi cha miaka minane na kuwatoa hofu watu wa Songea kwa kuwahakikishia kuwa kasi ya maendeleo katika jimbo lake haitapungua.
Uteuzi wa Dk Nchimbi na mawaziri wengine Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) ulitenguliwa mwishoni mwa mwaka jana baada ya malalamiko ya wabunge kutokana na matatizo yaliyojitokeza kwenye Operesheni Tokomeza.
CCM Dodoma waishukia Chadema
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma, Paul Luhamo amewataka wananchi wa Dodoma Makulu kukikataa Chadema kwa madai kuwa viongozi wake wanaendekeza malumbano ndani ya chama chao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo ya miaka 37 ya CCM katika Kata ya Dodoma Makulu, Wilaya ya Dodoma Mjini ambayo ni ngome ya Chadema, alitumia muda mwingi kuwaponda viongozi wa Chadema kuwa hawana jipya tena.
“Naomba mrudi CCM na kuweni na moyo wa kuchangia michango mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yenu na watoto wenu hata kama Kata hii inaongozwa na Chadema,” alisema Luhamo.
Moshi wamnadi mgombea
CCM Manispaa ya Moshi jana kilihitimisha sherehe za kuzaliwa kwa chama hicho kwa kumnadi mgombea udiwani Kata ya Kiboroloni, Willy Aidan.
Ujumbe wa viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwamo Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kijazi na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Moshi Mjini, Elizabeth Minde walimnadi mgombea huyo.
Katika mkutano huo uliofanyika eneo la Mnazi, kwa nyakati tofauti walisema maendeleo yanayoonekana sasa katika Mji wa Moshi yanatokana na sera makini za CCM.
Kijazi alisema haihitaji mtu kuwa na shahada kuweza kutambua maendeleo yaliyoletwa na CCM katika sekta za barabara, maji, afya, umeme na huduma za jamii tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Imeandikwa na Joyce Joliga, Sharon Sauwa na Daniel Mjema.
MWANANCHI