Quantcast
Channel: PAMOJA BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

UTEUZI WABUNGE WA KATIBA MFUPA MGUMU KWA JK

$
0
0
Rais jakaya Kikwete akitafakari jambo 
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete hataweza kukamilisha uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika muda wa wiki mbili kama ilivyokuwa imekadiriwa awali, kutokana na wingi wa majina yaliyopendekezwa kwa ajili ya uteuzi huo.
Ugumu wa mchakato wa uteuzi wa wajumbe hao unatokana na Rais Kikwete kupokea zaidi ya majina 5,000 yaliyopendekezwa na kuwasilishwa kwake kutoka taasisi na asasi mbalimbali za kijamii, huku yeye akitakiwa kuteua wabunge 201 tu, sawa na asilimia nne ya idadi ya majina yaliyopendekezwa.
Wateule hao wa Rais wataungana na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuunda  Bunge Maalumu la Katiba, ambalo linatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao mjini Dodoma.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameliambia gazeti hili kuwa ofisi yake ina kazi ngumu ya kuchagua majina ya wajumbe watakaoingia kwenye Bunge la Katiba na huenda kazi hiyo ikakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HI KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Balozi Sefue alisema Januari 15 iliyotajwa na Rais Kikwete yalikuwa ni makadirio tu ya awali, lakini kazi bado ni ngumu.
“Makadirio yangu ni mwisho wa mwezi huu (Januari). Ni kweli, Rais alitoa tarehe hiyo, lakini yalikuwa ni mapendekezo ya awali tu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:
“Hapa kuna mapendekezo ya vikundi zaidi ya 600 na kila kikundi kimetoa majina tisa; kwa hiyo kuna majina zaidi ya 5,400, kati yao tupate majina 200. Tunahitaji muda mrefu ili tufanye kazi kwa ufanisi.”
Desemba 13 mwaka jana, Rais  Kikwete alitoa tangazo kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2A) cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 akialika kila kundi kutoka pande zote za Muungano kuwasilisha kwake majina kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye uteuzi.
 Mgawanyo wa wajumbe
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe hivi karibuni kuwa makundi ya kijamii yalitakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya majina ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa mujibu wa sheria.
Alibainisha kuwa kila kundi linatakiwa kuzingatia umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu aliyependekezwa. Idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapungua moja ya tatu ya wajumbe wote.
Chikawe alisema wabunge hao 201 mchanganuo wao upo kwenye sheria na kwamba 20 watatoka kwenye taasisi zisizokuwa za kiserikali, ambapo nusu yao lazima wawe wanawake na moja ya tatu kutoka Zanzibar.
 Wengine ni wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
 “Vipo vyama 21 kwa maana hiyo, kila chama kitaleta wajumbe wawili, mgawanyiko ni huohuo, kwa hiyo kwa vyama vya siasa hapa lazima mmoja atoke Zanzibar na mwingine Bara na lazima mmoja awe mwanamke na mwingine mwanaume,” alisema Chikawe.
Wajumbe wengine na idadi yao kwenye mabano ni Taasisi za Elimu ya Juu (20), makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowawakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowawakilisha wavuvi (10) na vyama vya wakulima 20.
Mwakilishi wa Asasi
Mwakilishi wa Asasi za kiraia, Marcosy Albanie alisema kuwa tatizo la kufurika kwa majina linatokana na asasi nyingi kutokubali kuungana na kupeleka majina machache.
“Kuna jumla ya asasi za kiraia zaidi ya 66,000 nchini. Sisi katika muungano wa asasi za kiraia tulikubaliana tukutane Dodoma ili tuchague watu wachache. Lakini kuna taasisi zimejifungia ndani zikapeleka majina yao wenyewe kwa ubinafsi wao,” alisema Albanie na kuongeza: “Kazi hapo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, achukue majina ya taasisi tuliokaa Dodoma na kujadili kwa siku mbili, nyingine zikakaa zenyewe binafsi. Huo siyo utaratibu wa kidemokrasia.”
Akizungumzia utaratibu uliotumika kuwapata wajumbe hao, Albanie alisema kuwa wamechagua watu 40 yaani wanawake 20 na wanaume 20 kwa kujali usawa wa jinsia.
“Tumeangalia sekta 11, kanda tisa, maana tunataka kila kanda iwakilishwe. Katika kila kanda na sekta, majina ya watu wawili kwa aliyepata kura nyingi zaidi. Jina la mwanamke na mwanaume kwa kujali usawa wa jinsia. Pale tulipokosa mwanamke tumeweka wanaume wawili,” alisema Albanie.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema kuwa chama hicho kimezingatia sheria ilivyosema.
“Chadema tumepeleka majina kwa mujibu wa sheria. Sheria ilisema majina yasiyopungua manne na yasiyozidi tisa, tumefanya hivyo kwa kupeleka majina manne. Ikulu waeleze ni chama kipi au taasisi ipi iliyokiuka sheria na kivipi,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa chama hicho kilishatoa ushauri wa kurahisisha uteuzi ikiwa pamoja na Serikali kutaja makundi na majina ya taasisi.
“Ndiyo maana katika mapendekezo yao kwao juu ya muswada wa sheria, tulitaka siyo tu sheria kutaja makundi kwa jumla, bali pia majina ya taasisi zinazopaswa kufanya uteuzi na idadi ya wateule kwa kila taasisi,” alisema.
Hivi karibuni akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mnyika aliwataja waliopendekezwa kuwa ni Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Nasra Juma Burhan na Method Kimomogoro.
“Marando huyu ni msomi mwenye shahada ya Sheria na ni wakili wa Mahakama Kuu, Kimomogoro ni msomi wa sheria na ni Wakili wa Mahakama Kuu, Profesa Safari ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu aliyebobea kwenye mambo ya sheria, vilevile ni Wakili wa Mahakama Kuu na mama Burhani ni mwalimu kwa taaluma,” alisema Mnyika.
Chadema kimekuwa kikikosoa mchakato huo, hali iliyofanya mwaka 2012 kwenda Ikulu kukutana na Rais Jakaya Kikwete kikitaka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kubadilishwa. Baada ya chama hicho, vyama vingine navyo vilialikwa Ikulu na kuzungumza na Rais.
Naye Naibu Natibu Mkuu wa Cham cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema kuwa chama hicho kimefuata sheria ilivyosema kuwa majina yasipungue manne na yasizidi manne.
“Sisi tumefuata sheria ambayo ilitutaka tupeleke majina manne hadi tisa. Tumezingatia jinsi na ukanda kwa kuteua nafasi za wanaume sawa na wanawake. Hata hivyo, siwezi kukwambia idadi wala kutaja majina kwa sababu sera ya chama hairuhusu,” alisema Mtatiro.
 MWANANCHI

Viewing all articles
Browse latest Browse all 16395

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>