Naibu Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia, January Makamba.PICHA|MAKTABA
Mwanza. Katika kile kinachoonekana kama kujipigia debe katika kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewaambia viongozi wa dini Kanda ya Ziwa kwamba vijana wanapofika kuomba ridhaa yao, muwaangalie, msiwabeze.
Huku akikataa kuweka bayana nia yake ya kuwania urais kwa maelezo kwamba muda wa kufanya hivyo haujawadia, Makamba aliwaambia viongozi hao wa dini kwamba wagombea hao wanapopita wawasomee sifa za uongozi katika Biblia na kusema kumekuwapo mjadala wa sifa za uongozi kuhusu kijana na kusema amekuwa akitoa mwito kwa vijana wasiokuwa na makandokando kushiriki na kujitokeza katika kusaidia nchi ipone.
Akizungumza juzi usiku mjini hapa katika chakula cha pamoja na maaskofu na wachungaji kutoka Umoja wa Makanisa ya Kikristo wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli (CCM), alisema: “Huu ni wakati wa kila mmoja kutafakari hatima ya nchi yetu. Ndugu zangu… nadhani tuzungumze machache yanayohusu nchi yetu na Taifa letu, kwa sababu sote ni Watanzania na wote tuna hamu ya kujua na kutafakari mustakabali wa nchi yetu, umoja wetu, amani yetu na utulivu wetu.”
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema vijana wengi wamekuwa waoga kwa madai kwamba hawana fedha, uzoefu lakini akasema maaskofu na wachungaji wanapaswa kuwa mashahidi kupitia vitabu kwani katika Yeremia imeelezwa jinsi Mungu alivyompatia unabii Yeremia ambaye alidai yeye bado mdogo.
“Yeremia alipopewa unabii alilalamika mimi mdogo mimi siwezi, lakini Mungu alimwambiaje, ngoja nisome, (Yeremia 1: 4-10) …. Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nilikujua, kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalumu, nilikuweka uwe nabii kwa mataifa,” alisema na kuongeza:
“Bwana alimwambia usiseme, mimi ni mtoto mdogo. Utakwenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza, usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe.”
Alisema Tanzania inapita katika kipindi kigumu, hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuongoza maombi yatakayoiwezesha kupata kiongozi mwenye sifa ya kuivusha katika kipindi hicho.
Makamba amesema nchi inakabiliwa na nyufa kama vile rushwa, udini, ukabila, Uzanzibari na Uzanzibara, huku akirejea hotuba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya Machi 1995, ambayo aliyataja mambo hayo kuwa nyufa zinazoweza kuliangamiza taifa.
Alisema Tanzania inahitaji uponyaji na ikibidi kuanza upya kwa maana ya aina ya uongozi unaohitajika hivi sasa na kwamba ili kutimiza lengo hilo, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kutafakari na kuielekeza nchi njia sahihi ya kufuata.
“Shughuli za siasa zimeingiliwa na matapeli, lakini hata shughuli yenu pia imeingiliwa na matapeli. Sasa tunapotafuta uponywaji wa nchi yetu ninyi mna nafasi kubwa kwani uponyaji tunaouzungumzia ni wa maovu ya kiroho, uongo, ubakaji na vitu kama hivyo, ninyi mna nafasi kubwa sana,” alisema.
Alisema viongozi wa kisiasa pia wanayo nafasi yao katika kuponya taifa lakini lazima wanapofanya kazi hiyo wawe wasafi.
Alisema askofu au mchungaji akihubiri anapaswa kuwa msafi na hata katika uongozi wa siasa anaposimama mtu na kusema yeye ni jawabu la matatizo ya wananchi ni vizuri kumtazama sura yake kama ameacha (maovu).
“Tunapoomba uongozi wa kisiasa zipo sifa kwani tunaomba kuongoza watu wa Mungu ambao ni walewale wanaokuja kanisani ndiyo wanaokuja katika siasa, kuongoza watu wa Mungu siyo kitu kidogo…… hivyo lazima vigezo vya kuongoza watu hawa viwe vikubwa sana,” alisema.
Rasilimali za nchi
Alisema Tanzania hivi sasa inakabiliwa na changamoto zinazoweza kuitwa kuwa ni za kidunia na za kibinadamu zinazojumuisha masuala kama vile upatikanaji wa huduma za afya, maji na elimu.
“Tunagawanyika ingawa migawanyiko hiyo si ya kidini, rangi na kikabila... iko ya namna gani, watu wachache wananufaika na keki (rasilimali) ya taifa kuliko wengine,” alisema Makamba na kuongeza:
“Sasa Serikali, hili kwetu ni muhimu sana…. hakuna kitu muhimu kama kuendelea kujenga umoja wa taifa letu, migawanyiko hii ndiyo changamoto. Elimu anayoipata mtoto wangu ndiyo anaipata mtoto wa Rwamgasa, Kwimba na Nyarugusu?”
Alisema usawa katika elimu pamoja na huduma nyingine kama afya na nyingine muhimu, ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa lenye amani na umoja kwani kila mmoja atajihisi kunufaika na rasilimali za nchi.
Naibu Waziri huyo alisema changamoto nyingine zinazoikabili nchi ni vitendo vya rushwa, ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, ubakaji, utapeli na kuporomoka kwa maadili.
Alisema taifa halipaswi kusubiri adhabu kutoka kwa Mungu kama inavyosomeka katika vitabu vitakatifu ambako kuna ushahidi kuhusu gharika wakati wa Nuhu, pia moto wakati wa Sodoma na Gomora, huku akiwapa changamoto viongozi wa dini kukabiliana uovu unaoshika kasi.
“Sasa taifa letu lina miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika na mwakani tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Zanzibar. Miaka 50 ni mingi kwa binadamu, lakini ukweli ni kwamba kazi ya kulijenga taifa letu ndiyo inaanza.”
Shinikizo la maaskofu
Baada ya hotuba yake, baadhi ya maaskofu na wachungaji walisikika wakimshinikiza Makamba atangaze nia ya kugombea urais lakini alisema atafanya hivyo wakati mwafaka ukiwadia.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa hayo ya Kikristo, Askofu Charles Sekelwa alisema: “Viongozi wa dini tukubaliane kuwa walezi na tusimkatae mtu kwa dini yake wala kabila lake. Wakijitokeza vijana huko mbele tuwaunge mkono, hayo maneno ni ya mtu mwenye hekima”.
Askofu Jacob Lutabija alisema amepokea ujumbe mzito ambao atakwenda kuutangaza kwa waumini wake wa Musoma akisema kwa watu wenye hekima zao wametambua nini wanapaswa kufan
MWANANACHI
Askofu Jacob Lutabija alisema amepokea ujumbe mzito ambao atakwenda kuutangaza kwa waumini wake wa Musoma akisema kwa watu wenye hekima zao wametambua nini wanapaswa kufan
MWANANACHI