Takriban watu 22 wameripotiwa kufariki katika milipuko miwili ambayo ililenga ubalozi wa Iran mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon
Picha nyingi za mashambulizi hayo zilionyesha magari yakiteketea pamoja na miili ya watu ikiwa imetapakaa kwenye barabara za eneo hilo. Majumba pia yaliharibiwa vibaya.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFA HAPA CHINI
Afisaa mmoja mkuu katika ubalozi huo Ebrahim Ansari alikuwa miongoni mwa waliofariki. Maafisa wamesema kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka
Iran inaunga mkono kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Hezbollah ambalo limewapeleka wapiganaji nchini Syria kuunga mkono serikali ya Rais Bashar al Assad.
Duru zinasema kuwa moja ya milipuko hio, ilisababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga, wakati shambulio la pili lilitokana na bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari.
Shirika la habari la Reuters linanukuu kituo cha televisheni cha CCTV, kikionyesha mwanamume mmoja akikimbia kutoka katika ubalozi wa Iran na kisha kujilipua
Syria imelaani vikali mashambulizi hayo. Mgogoro wa kisiasa nchini Syria umechochea kuongezeka kwa hali ya wasiwasi nchini Lebanon.
Balozi wa Iran nchini Beirut alithibitisha kifo cha bwana Ansari, ingawa haijulikani ikiwa alikuwa ndani ya ubalozi au katika jengo jirani