Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Watu watano wamejeruhiwa kwa kushambuliwa na viboko kwa nyakati tofauti katika bwawa la Mtera mkoani iringa na wawili kati yao kulazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa huo matukio yanayodaiwa kuongezeka kufuatia ongezeko la wanyama hao kwenye bwawa la mtera. Majeruhi hao Agustino Kinyaga na Sunday Ngonyani ambao ni wavuvi wamesimulia jinsi walivyovamiwa na kushambuliwa na viboko hao na kuiomba serikali kutazama uwezekano wa kuwapunguza kwa kuwavuna ili kupunguza adha hiyo.
Muuguzi wa zamu katika wodi ya majeruhi hospitali ya rufaa ya mkoa wa iringa Bibi Beatrice Livigha amesema waliwapokea majeruhi hao kati ya tarehe 28 na 30 mwezi huu wakiwa katika hali hiyo na kuwaanzishia matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Kaimu afisa wanyama pori wilaya ya iringa Bi.Fatuma Juma amesema wamepewa taarifa za kujeruhiwa kwa watu hao na kwamba wameshapata malalamiko ya ongezeko la viboko na mamba katika Bwawa hilo lakini kwakuwa mchakato wa kuvuna wanyama hao unaihusu zaidi wizara ya maliasili na utalii ofisi yake imechukua hatua za dharula kwa kutuma askari kufanya doria bwawani mtera ili kudhibiti hali hiyo.
CHANZO: ITV TANZANIA