Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma DAVID MISIME - SACP akiongea na akinamama wa kituo hicho.
Mkuu wa kituo cha CHIKANDE Afisa Muuguzi DAINESS TUNI akiongea katika Maadhimisho hayo.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma DAVID MISIME - SACP akiteta jambo na Mkuu wa Kituo hicho Nesi DAINESS TUNI wakati wa maadhimisho hayo.
Washiriki wa maadhimisho wakisikiliza mawasilisho ya mada mbalimbali.
Kamanda wa Polisi Mkoa DAVID MISIME - SACP akimkabidhi zawadi kwa Afisa Muuguzi GLADNIS TUMBO wa kituo hicho.
Muonekano wa ndani ya Wodi ya akinamama wa kituo cha CHIKANDE wakiwa vitandani na wengine chini kwa kukosa vitanda wakisubiri siku zao za kujifungua.
Akinamama wanaotarajia kujifungua wakiwa katika maadhimisho hayo wakimsikiliza mgeni rasmi.
Stori na: Sylvester Onesmo, picha na Dorice Kigombe wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanya maadhimisho ya kilele cha kufunga siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Kilele cha maadhimisho hayo yalianzia katika kituo cha CHIKANDE kinachohifadhi akina mama wajawawito wanaosubiri muda wa kujifungua ambacho kipo chini ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kuhitimishwa kwa mdahalo maalumu katika ukumbi wa bwalo la Polisi Dodoma. Wanawake hao ni wale ambao wamepata mimba katika umri mdogo, wenye mimba zenye matatizo wakati wa kujifungua pamoja na wanawake ambao wamezaa mara nyingi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema maadhimisho haya yalianza tarehe 25/11/2014 hadi tarehe 10/12/2014 yakiwa na lengo la kupinga unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii ngazi zote juu ya uwepo wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha harakati dhidi ya kupinga unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kamanda MISIME alisema maadhimisho hayo yanalenga kuunganisha harakati za ndani na dunia kwa ujumla sambamba na kutoa furlsa ya majadiliano ya pamoja na kushirikishana katika mikakati mbalimbali pamoja na kushawishi serikali ili ijaribu kutekeleza maazimio ya kisheria yaliyofikiwa kitaifa na kimataifa katika kuwalinda wanawake na watoto.
Aidha Kamanda MISIME alisema, Madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni pamoja na Vifo, Ulemavu, Familia kuvurugika, Kuathiliwa kwa taaluma za wanafunzi, Kuambukizwa magonjwa mbalimbali, Mimba zisizotarajiwa, Kuwepo kwa misongo ya mawazo, Kuathiriwa kisaikolojia, kuwepo kwa ubaguzi baina ya watoto wa kike na kiume katika ngazi ya familia katika kupata elimu, urithi vile vile kuozwa watoto wa kike wakiwa na umri mdogo.
Akisoma risala kwa niaba ya Wanatandao Polisi Wanawake Mkoa wa Dodoma – TPF Net, Mkaguzi msaidizi wa Polisi IVONIA MDENYE alisema tunapofanya maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto kwa vitendo, pia tunafanya matendo ya huruma kujali wahitaji mbalimbali katika hali na mali.
Alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilitoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulea watoto waishio katika mazingira magumu cha SAFINA STREET CHILDREN kilichopo eneo la Air Port siku ya ufunguzi tarehe 25/11/2014 na tena siku kilele cha maadhimisho ya siku 16 kwa kutembelea kituo cha wajawazito cha CHIKANDE kushiriki maadhimisho kwa pamoja, kutoa elimu, pamoja na kutoa zawadi ambazo ni mguso wa watu binafsi askari Polisi wakiamini kwamba nasi tulizaliwa na akina mama wenye shida kama wengine.
Nae Mkuu wa kituo cha CHIKANDE Afisa Muuguzi DAINES TUNI amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanya maadhimisho hayo katika kituo hicho na kusema, akina mama hao ni kutoka vijijini wako mbali na familia zao, kutembelewa huko ni faraja kwao. Pia alisema kituo hicho kilijengwa mwaka 1992 kwa madhumuni ya kuwasaidia akinamama wajawazito wanaotarajia kujifungua kuwa karibu na huduma na ushauri wa kiafya kwa mama mjamzito. Alisema katika kituo hicho wapo wenye umri mdogo ambao wanatarajia kujifungua uzao wa kwanza na wenye uzao mwingi zaidi ya watoto 12.
Kituo hicho kina miaka 22 tangu kianzishwe, kinakabiliwa na changamoto ambazo ni upungufu wa vitanda kwani kituo hicho kinauwezo kuhudumia akinamama 15 lakini mpaka sasa kituo hicho kina akinamama 74, lakini wakati mwingine hufikia watu zaidi ya 100 wanotarajia kujifungua wakitokea maeneo ya nje ya Manispaa ya Dodoma. Vilevile Afisa Muuguzi huyo aliiomba serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kusaidia kituo hicho kwa karibu hasa kwa suala la usafiri wa kuwasaidia akina mama hao wanapozidiwa kwa uchungu kuwapeleka Hosipitali ya rufaa ya Dodoma kwa kujifungua.