Polisi nchini Kenya wanasema kuwa wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al Shabaab wamewauwa kwa kuwapiga risasi zaidi ya watu 28 waliokuwa wakisafiri kwenye basi moja karibu na mpaka wa Somalia.
Maafisa wa ngazi ya juu wamesema kuwa basi hilo lilitekwanyara katika Jimbo la Mandera wakati likiwa njiani kuelekea katika mji mkuu Nairobi.
Watu wasiokuwa waislamu wanasemakana kutengwa na abiria wengine na kisha kupigwa risasi.
Kundi la al-Shabab nchini Somalia limetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Kenya tangu mwaka 2011.
Huo ndio mwaka ambapo Kenya iliwatuma wanajeshi wake nchini Somalia kupigana na kundi hilo la waislamu wenye itikadi kali.
Mji wa Mandera katika eneo la Kaskazini mashariki ndio ulioathirika pakubwa. Baada ya shambulio hilo la mapema jumamosi maafisa katika eneo hilo wamenukuliwa na vyombo vya habari nchini kenya wakisema kuwa serikali ilikataa kuitikia ombi lao la kutaka usalama kudumishwa zaidi.
Afisa mmoja ameliambia gazeti la Daily Nation kwamba wavamizi hao waliwataka abiria kusoma aya katika Koran kabla ya kuwaangamiza walioshindwa kufanya hivyo.
CHANZO: BBC SWAHILI