Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepanga kusikiliza maelezo ya awali dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee (35) na wenzake wanane wa Chama Cha Demekrasia na Maendeleo wanaokabiliwa na mashitaka ya kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko isivyo halali kwa lengo la kwenda Ikulu.
Kesi hiyo ilitajwa leo na Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda.
Mbali na Mdee, washtakiwa wengine ni, Rose Moshi (45), Renina Peter, Anna Linjewile (48), Mwanne Kassim (32), Sophia Fangel (28), Edward Julius (25), Martha Mtiko (27) na Beatu Mmari (35), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Hellen Moshi alidai kuwa washtakiwa wote wapo na upande wa Jamhuri unaomba tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.
Hakimu Kaluyenda alisema kesi hiyo itasikilizwa Novemba 16, mwaka huu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa, Oktoba 4, mwaka huu washtakiwa wakiwa Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf, kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 124 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la pili washtakiwa hao wakiwa eneo hilo hilo, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo moja la kutembea kwenda Ofisi ya Rais, huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Wakili huyo alidai kuwa, kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 74 na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao, walikana kuhusika na tuhuma hizo.