Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye kambi za watalii katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo katika mikoa ya Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani akiwa katika baa maarufu ya Arusha Raha iliyopo la Shams, jijini hapa.
Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya kuligonga gari jingine katika eneo la Mbauda wakati akitokea katika makazi yake yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa maarufu ya Arusha Raha.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo baada ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa wamemzingira katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari lake aina ya Nissan Navara.
“Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguza wakanywea, akatumia mwanya huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la kujificha, na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa haraka pombe mbili kali aina ya Valuer na wakati anamalizia ya tatu, akajikuta anazingirwa tena na wale waendesha bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili nyingine hewani, lakini bila ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo akaamua kujimiminia risasi.
Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi wasamaria wema wakiwa harakati za kupiga simu polisi walishitukia polisi wakiingia katika eneo la tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia risasi kifuani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ingawa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha imekiri kuwepo kwa tukio, lakini chanzo chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji wa matukio ya jeshi hilo mkoani Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.