Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Mgeni Rasmi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mwantumu Mahiza (aliyesimama) akisisitiza jambo alipokua akifungua kikao cha Baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi Ofisi ya Rais, Tume ya Mipando kwa pamoja wakiimba wimbo wa Solidarity Forever kuonyesha mshikamano makazini.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakionyesha mshikamano kwa kuimba wimbo wa Solidarity forever mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kufungua rasmi kikao hicho.
Kabla ya kuanza majadiliano, wajumbe walimchagua Mwenyekiti Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi ambapo Bibi Magreth Simwela (aliyesimama) aliibuka mshindi kati ya wajumbe watatu waliokua wakigombea nafasi hiyo. Hapo Mwenyekiti Msaidizi alikua akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza (Walioketi wa pili kushoto). Walioketi pamoja nae kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bibi Florence Mwanri, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mipango, Bw. Steven Katemba na Katibu wa Baraza Bw. Senya Robert.
...............................................................
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA PWANI MH. MWANTUMU BAKARI MAHIZA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO KATIKA UKUMBI WA HOTELI YA JD COMPLEX – KIBAHA, PWANI.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa leo hii tukiwa na afya njema. Pia, nikushukuru wewe binafsi Kaimu Katibu Mtendaji, pamoja na timu yako kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Ndugu washiriki,
Nimearifiwa kuwa Baraza hili ni la kwanza katika mwaka 2014/15 na limewakilishwa na Wakuu wote wa Klasta, Idara na Vitengo, wajumbe wa TUGHE Taifa, TUGHE Mkoa – Dar es salaam, Halmashauri ya Tawi la TUGHE Tume ya Mipango na mjumbe mmoja mmoja kutoka kila Klasta, Idara na Vitengo.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wote wa mkutano huu kwa kuchaguliwa kwenu kuwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kupitia mabadiliko ya Mkataba Mpya. Hii ni kutokana na imani kubwa waliyonayo watumishi juu yenu katika kuwawakilisha katika chombo hiki muhimu.
Ndugu washiriki,
Baraza la Wafanyakazi ni kama Bunge la Taasisi yenu kwa kuwa linaundwa na wawakilishi wa wafanyakazi wote waliochaguliwa kidemokrasia. Baraza hili ni chombo muhimu sana kilichoundwa kisheria kwa madhumuni ya kuwashirikisha watumishi katika kujadili na kufanya maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya ajira mahali pa kazi kwa lengo la kuleta tija. Kupitia Baraza hili mwajiri anapokea maoni ya watumishi na kuweza kufikia maamuzi sahihi ya namna ya kuboresha mazingira ya kazi na watumishi kwa ujumla.
Wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi yenye tija.
Ndugu washiriki,
Hata kama kutakuwa na sera, sheria na kanuni nzuri katika mahali pa kazi pasipokuwa na ushirikiano baina ya mwajiri na watumishi itakuwa vigumu Taasisi kutimiza malengo yake. Hivyo pamoja na mambo mengine Baraza hili lina wajibu wa kuishauri Tume kwa lengo la kuleta tija na mshikamano baina ya mtumishi na mwajiri. Sio vizuri kwa watumishi kutumia muda mwingi katika kudai maslahi zaidi kuliko kupima kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao.
Moja ya kazi za Baraza ni kuhakikisha kuwa watumishi wanatekeleza wajibu wao kwanza kabla ya kudai maslahi na wanapodai maslahi wanatakiwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zilizopo.
Ndugu washiriki,
Tume ya Mipango iliundwa chini ya Ofisi ya Rais kutekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kutoa dira ya maendeleo na mwongozo wa uchumi wa taifa, kubuni na kuishauri Serikali kuhusu sera za menejimenti ya uchumi na mikakati ya maendeleo na kufanya utafiti.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Napenda kutumia nafasi hii kukupongeza Mwenyekiti kwa kushirikiana na wasaidizi wako na watumishi wote kwa ujumla kwa kuweza kutekeleza majukumu mliyopewa kitaifa kwa ufanisi. Nimeelezwa kuwa pamoja na changamoto za uhaba wa rasilimali katika mwaka wa fedha 2013/14 mmeweza kutekeleza jukumu kubwa la kutayarisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa, 2014/15 ambao uliwasilishwa katika kikao cha Bunge cha mwezi Juni 2014, pamoja na majukumu mengine ambayo ni kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), kusambaza machapisho mbalimbali ya Tume ya Mipango na kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management Manual).
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Ni matarajio yangu kuwa kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Serikali, Tume ya Mipango mmepanga malengo mbalimbali ya kutekeleza katika mwaka wa 2013/14 ambapo hatimaye mtakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwa kusema hivi natumaini kuwa michango yenu katika mkutano huu wa siku mbili, itatoa matokeo makubwa yatakayoliwezeshaTaifa letu kusonga mbele kiuchumi.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Hivyo, ni matumaini yangu kuwa kwa kutumia kikao hiki kama wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi mnayo nafasi kubwa ya kuwaelimisha wafanyakazi wenzenu kuhusu umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika sehemu yake ya kazi ili kufikia malengo mliojiwekea. Njia pekee ya kufikia malengo yetu ni kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kulitendea haki Taifa letu. Kila mmoja wetu akemee kwa sauti watumishi wasiotimiza wajibu wao. Wakuu wa Klasta, Idara na Vitengo wasimamie kwa dhati suala la maadili katika sehemu zao za kazi. Tukumbuke kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huelekeza kuwa kila mtu apate ujira unaolingana na wajibu aliotimiza.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Nimeelezwa kwamba miongoni mwa mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huu ni mafanikio ya utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2013/14 na kujadili taarifa ya fedha za mwaka, elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, umuhimu wa mawasiliano serikalini na uelewa juu ya kiwango kinachopaswa kutozwa kodi ya mapato yatokanayo na ajira (mshahara).
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Mwisho napenda kutoa shukrani kwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huu muhimu na kuwatakia majadiliano mazuri na yenye lengo la kuimarisha uhusiano mzuri kwenye Taasisi yenu. Nihitimishe kwa kuwatakia kikao chenye mafanikio yaliyokusudiwa.
Baada ya kusema hayo machache, napenda kutamka kwamba ‘Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Mipango Umefunguliwa Rasmi’!