Watuhumiwa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wakiwa katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, walipofikishwa na kusomewa mashtaka.
Haya ni majina ya watuhumiwa ya mauaji
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Dar es Salaam. Watu 10 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kumuua kwa kukusudia Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi.
Akiwasomea shtaka hilo jana, Wakili wa Serikali, Aida Kisumo aliwataja washtakiwa hao, Chibago Magozi (32) mfanyabiashara na mkazi wa Vingunguti Machinjioni, John Mayunga (56) mfanyabiashara na mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29) na Masunga Makenza (40) dereva na mkazi wa Kitunda, ambaye anatuhumiwa kuwa ni kibaka mzoefu.
Kisumo aliwataja watuhumiwa wengine, Paulo Mdonondo (30) mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40) Mkazi wa Vingunguti, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni, Msungwa Matonya (30) mkazi wa Vingunguti na Ahmad Kitabu (30) mkazi wa Mwananyamala wilayani Kinondoni.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja Novemba 3, mwaka huu walifanya kosa hilo la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kisumo alidai kuwa siku ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa shtaka hilo, Hakimu Sundi Fimbo aliwataka wasijibu kitu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kulisikiliza shtaka hilo hadi Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana na upelelezi bado haujakamilika, washtakiwa walipelekwa rumande hadi Desemba 5, mwaka huu itakapotajwa.
Washtakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi na baada ya kesi, waliondoka kwa kutumia gari aina ya Land Cruiser KX 06 EFD ambalo lilikuwa likisindikizwa na gari aina ya Noah namba T 539CCB.
MWANANCHI
MWANANCHI