Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma David Misime - SACP
Na: Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linafanya uchunguzi wa kifo cha SAFELA D/O ANDREW mwenye umri wa miaka 18, Mgogo, Mkristo Mkazi wa Area C aliyekuwa anafanya kazi za ndani kwa JACKSON S/O JUMA @ COY mwenye umri wa miaka 35, Mjaruo, Mkazi wa Area C Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP amesema binti huyo amegundulika akiwa amekufa katika pagale (nyumba ambayo haijamalizika) tarehe 22/07/2014 majira ya 08:00hrs.
Kamanda MISIME amesema kulingana na uchunguzi wa awali binti huyo alitoweka nyumbani kwa tajiri yake toka tarehe 19/07/2014.
Aidha kulingana na maelezo ya tajiri yake anasema kuwa waliporudi nyumbani toka kazini majira ya saa 21:00hrs hawakumkuta binti huyo na wakafanya jitihada za kumtafuta kwa majirani na sehemu mbalimbali lakini hakuonekana.
Aliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa eneo la Area C na kituo cha Polisi.
Kamanda MISIME amesema maiti ya msichana huyo imehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa Mkoa wa Dodoma ikisubili uchunguzi wa madaktari kubaini chanzo cha kifo chake kwani mwili wake ulishaanza kuharibika.