WATU watatu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi wameuwawa jijini Arusha walipokuwa katika harakati ya kwenda kupora mamilioni ya fedha zilizokuwa zinapelekwa benki na kampuni ya Arusha Islamic Centre inayohusika na utengenezaji na uuzaji wa vigae iliyopo eneo la Esso mjini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Arusha leo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas amesema kuwa,majambazi hao watatu waliuawa jana tarehe 3 eneo la TBL -Njiro wakiwa kwenye harakati za kwenda kupora fedha hizo.
Alisema kuwa, majambazi hao walikuwa mahali wanapanga njama majira ya saa 4;20 asubuhi wakisubiria kuteka gari lililokuwa limebeba fedha zilizokuwa zinapelekwa benki zaidi ya milioni 100 huku wakiwa na gari aina ya Toyota Corola yenye namba za usajili T 762 CWE.
Alisema kuwa, raia wema walitoa taarifa kuhusiana na tukio hilo ndipo polisi walifika eneo ambalo majambazi hao walikuwa wamejificha katika eneo la unga ltd relini ambapo majambazi hao walishtuka na kuanza kuirishia gari hiyo ya polisi risasi.
Kamanda Sabas alisema kuwa,Askari wake walioona Majambazi hao wanawamiminia risasi kama mvua,ndipo na wao walipojibu mashambulizi na na kufanikiwa kuwawa kwa majambazi hao watatu na kufanikiwa kuchukua silaha yao aina ya shortgun yenye namba A 947514 M aina ya Pumpaction ikiwa na risasi 3 .
Kamanda alisema kuwa, bado majina ya majambazi hayo hayajafahamika ambapo wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya mount Meru.
Aidha Kamanda aliwashukuru wananchi kwa juhudi kubwa sana walizoonyesha na ushirikiano hadi kukamatwa kwa majambazi hayo na kuwataka kuendelea kuongeza juhudi hizo zaidi.