Aliyekuwa Mtayarishaji Vipindi na Muongozaji wa filamu, Marehemu George Tyson aliyefariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro(May 30) ataagwa katika viwanja vya Leaders Club Jumanne (Juni 3) na baada ya hapo mwili kusafirishwa kwenda nchini Kenya kwaajili ya maziko.
Akizungumza na mtandao huu leo mwenyekiti wa Bongo movie, Steve Nyerere, amesema baada ya kuwasili kwa mwili wa marehemu ataagwa Leaders Club na baada ya hapo mwili utasafirishwa kupelekwa Kenya.
“Tunashukuru Mungu mwili wa George Tyson umewasili jana Dar es salaam ukitokea mkoani Morogoro na mwili umehifadhiwa katika hospitali ya Kairuki, kumuaga marehemu itakuwa Leaders Club siku ya Jumanne na baada ya kuuaga mwili utasafirishwa Kenya kwa mazishi,”alisema.
George Tyson alipoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Gairo akiwa safarini kurejea Dar es Salaam akiwa na timu ya kipindi cha The Mboni Show. Sababu ya ajali hii imeelezwa kuwa ni tairi ya gari kupasuka na kusababisha gari kupoteza muelekeo na kupinduka. Gari hiyo ilikuwa na watu nane ndani yake ambapo George peke yake ndiye aliyepoteza maisha na wengine kujeruhiwa.