Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao akiwasha Mshumaa wa Pasaka wakati wa Misa ya mkesha wa Pasaka uliofanyika kwenye Kanisa la Kuu la Makatifu Joseph, Zanzibar jana. Picha na Martin Kabemba
Ni katika waraka maalumu unaoitwa ‘Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.
Maaskofu 32 wa Kanisa Katoliki Tanzania, wametoa waraka maalumu wa Pasaka wakiwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuweka pembeni itikadi za kisiasa katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Kupitia tamko lao la pamoja walilolitoa jana na kulipa jina la “Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema,” maaskofu hao walisema hivi sasa kuna makundi yenye nguvu ambayo yameanza kushinikiza kuingizwa mambo yenye masilahi kwao kwenye Katiba Mpya.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
“Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania,” walisema katika tamko hilo ambalo, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alithibitisha kuwa umetolewa na kanisa hilo.
Kauli ya viongozi hao ambayo ilisomwa katika makanisa mbalimbali nchini jana, imekuja ikiwa zimepita siku sita tangu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kutokana na mvutano unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa Serikali.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo kumekuwa na mvutano kuhusu muundo wa Serikali, huku CCM kikiupinga muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutaka muundo wa serikali mbili, ambao unapingwa na upinzani.
“Kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na haishangazi kuona migongano ya hoja kwa makundi kinzani. Mawazo ya wengi yamewasilishwa kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba,” inasomeka sehemu ya tamko hilo ambalo limechapishwa kwa ukamilifu katika ukurasa wa 6 wa gazeti hili na kuongeza:
“Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile ili kujihakikishia kuendelea kulinda masilahi yake ya kisiasa.”
Maaskofu hao ambao majina yao yameorodheshwa kwenye waraka huo, wamewataka wajumbe wa Bunge hilo kuachana na itikadi za kisiasa ili kufikia mwafaka katika masuala muhimu yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo kwa manufaa ya wote.
Huku wakitolea mfano umoja, amani na utulivu nchini ambao umekuwa kimbilio kwa mataifa mengine, walisema hivi sasa kuna dosari kadhaa katika umoja wa Watanzania.
“Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndiyo ukweli,” walisema.
Walisema kasoro zilizojitokeza katika mambo mbalimbali ndiyo chanzo cha watu kutaka mabadiliko: “Watu wengi walitaka na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi. Kwa msukumo huo ndiyo sababu ya kuingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.”
Walisema Watanzania hawatakiwi kukata tamaa, huku wakiwakata watu wenye nia njema kushirikiana na kupambana na nguvu za maovu na ubinafsi na kuachana na itikadi za kisiasa ili kupigania haki za wanyonge.
“Tuandae Katiba ambayo itatupatia misingi imara ya maadili itakayotuongoza kupigana dhidi ya ubinafsi na ufisadi na kutetea haki za binadamu kwa wote,” walisema.
Hata hivyo, walisema iwapo utakuwapo muafaka na kukubaliana katika mambo muhimu kwa maisha ya mshikamano wa kitaifa ambayo katika Rasimu ya Katiba yameandikwa kwenye sura ya kwanza hadi ya tano, muundo wowote wa serikali unawezekana.
Walisema ili kufikia lengo la kuwa na Katiba bora ni lazima maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe kama ambavyo imetamka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kuwe na nia njema ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji katika dola zilizopo katika Muungano, kutokuwa wabinafsi pamoja na kuchambua matatizo ya sasa ya Muungano na kuridhia mfumo utakaomaliza matatizo hayo,” walisema.
Akizungumzia waraka huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema ameusikia ukisomwa na Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar na kuelezea kufurahishwa na yaliyomo.
Malasusa aonya
Kwa upande wake Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa alisema wanasiasa wanatakiwa kutambua kuwa Katiba Mpya si mali yao, bali ya Watanzania wote.
Akizungumza katika ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front jana Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema: “Katiba Mpya itapatikana kama watu wakiheshimiana, kuridhiana na kuaminiana. Waliapa kufanya kazi bila upendeleo na hilo ni lazima walizingatie.”
Alisema kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na kwamba licha ya misuguano ya wajumbe wa Bunge hilo bado wanatakiwa kuweka tofauti zao za kisiasa pembeni na kufikiria mustakabali wa taifa.
“Hatupendi kuona kundi lililoshindwa na lililoshinda. Tunachotaka kukiona ni Katiba itakayowaweka Watanzania pamoja,” alisema.
Ibada hiyo iliyofanyika kitaifa katika kanisa hilo ilihudhuriwa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu.
MWANANCHI